Monday, December 23, 2024
spot_img

ANGELLAH KAIRUKI AMESHIKA NDOTO YA RAIS SAMIA YA 2025  

MAKALA MAALUMU

NDOTO ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuongeza idadi ya watalii nchini hadi kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2025 na pato la Taifa linalotokana na utalii kufikia Shilingi bilioni sita kwa mwaka, imeshikwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki.

Yakini Waziri Kairuki ameishika vema ndoto ya Rais Samia na ameitafasri vema kwenye hotuba ya mpango wa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2024/2025 ya Wizara ya Maliasili na Utalii, aliyoisoma kwenye Bunge la Bajeti.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angella Kairuki (kulia) akizungumza na Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta bungeni Dodoma.

Juni 7, 2022 Rais Samia akiwa kwenye Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara, aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kukutana na wadau wa Sekta ya Utalii kujadili mapendekezo ya mageuzi ya sera, sheria, taratibu na kanuni ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta hiyo ili kufikia lengo la kuongeza watalii wanaotembelea nchini hadi kufikia milioni tano, mwaka 2025 sambamba na mapato yatokanayo ya biashara ya utalii.

Rais Samia Suluhu Hassan akiongoza Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara.

Katika kutekeleza maagizo hayo ya Rais Samia. Waziri Kairuki anaeleza Bunge na Taifa kuwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambalo ni muhimili muhimu wa Sekta ya Utalii nchini, limevutia watalii kutoka pande mbalimbali duniani kutembelea Hifadhi za Taifa.

Akitoa takwimu, anasema hadi Aprili 2024, watalii 1,598,608 walitembelea Hifadhi za Taifa. Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 11.4 ikilinganishwa na watalii 1,435,069 waliotembelea Hifadhi za Taifa mwaka wa fedha 2022/2023.

Wabunge wakitekeleza majukumu ya kibunge kwenye ukumbi wa Bunge Dodoma

Akizungumzia ongezeko la mapato yatokanayo na utalii, Waziri Kairuki anasema TANAPA limekusanya mapato ya Shilingi 353,441,080,170.15 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 21.58 ikilinganishwa na mapato ya Shilingi 290,698,543,140.17 zilizokusanywa kwa kipindi kama hicho, mwaka wa fedha 2022/2023.

Katika hotuba yake hiyo, Waziri Kairuki anazungumzia pia uimarishaji miundombinu akisema kuwa TANAPA chini ya miongozo na maelekezo ya Serikali limeimarisha na kuendeleza miundombinu ya utalii kwa kufungua barabara mpya zenye urefu wa kilometa 694.5 katika Hifadhi ya Taifa Nyerere.

Uwanja wa ndege uliopo Hifadhi ya Taifa Nyerere.

Pia TANAPA limejenga vituo nane vya askari katika Hifadhi za Taifa Nyerere, Mto Ugalla, Burigi-Chato, Ruaha, Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe na pia limejenga nyumba 29 za watumishi katika Hifadhi za Taifa Nyerere, Ruaha, Mkomazi, Mto Ugalla, Gombe na Tarangire.

Anasema kwa kuzingatia kauli mbiu ya Rais Samia isemayo ‘kazi iendelee,’ TANAPA limekarabati barabara zenye urefu wa kilomita 3,631 katika Hifadhi za Taifa Arusha, Ziwa Manyara, Katavi, Kilimanjaro, Tarangire, Ruaha, Saadani, Burigi-Chato, Mikumi, Rumanyika-Karagwe, Serengeti na Mkomazi pamoja na njia za kupandia milima zenye urefu wa kilomita 157.

Waziti Kairuki anasema TANAPA limekarabati viwanja vya ndege 12 katika Hifadhi za Taifa Nyerere, Serengeti, Katavi, Tarangire na Mkomazi na pia ujenzi unaendelea wa viwanja vya ndege vinne katika Hifadhi za Taifa; Ruaha vipo viwanja viwili, Mikumi kiwanja kimoja na Nyerere kiwanja kimoja.

Kuhusu utendaji kazi, Waziri Kairuki anasema TANAPA limeendelea kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa kuboresha huduma kwa watalii na watumishi na limejenga mfumo wa usambazaji maji safi kwa watumishi katika Hifadhi ya Taifa Ruaha malango mapya vinne; katika Hifadhi za Taifa Nyerere kimoja, Mikumi viwili na Ibanda Kyerwa kimoja na ujenzi wa Ofisi ya Utawala Kanda ya Kusini.

Hifadhi ya Taifa Serengeti

“Vilevile, Shirika liko katika hatua ya ukamilishaji ujenzi wa malango manane katika Hifadhi za Taifa Tarangire – lango la Mamire, Ibanda-Kyerwa – lango la Kifurusa, Nyerere – lango la Msolwa na Likuyu, Mikumi – lango la Kikwaraza na Doma pamoja na Serengeti – lango la Kleins na Machochwe,” anasema.

Hotuba ya Waziri Kairuki inazungumzia pia uimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji maduhuli katika malango yote ya Hifadhi za Taifa ikiwemo uwekaji wa mifumo ya malango janja (smart gates) katika Hifadhi za Taifa Serengeti mifumo mitatu, Ziwa Manyara mfumo mmoja na Tarangire mifumo miwili.

Anazungumzia ukuzaji utalii kwa kueleza kuwa TANAPA limeendelea kushiriki na kushirikiana na wadau wa utalii katika kuandaa maonesho na matukio mbalimbali ikiwemo ushiriki wa Ruaha Great Marathon pamoja na matukio mbalimbali ya kimichezo yaliyoratibiwa na wizara.

Na kwamba kwa upande mwingine, Hifadhi ya Taifa Serengeti imeendelea kupokea tuzo za Africa’s Leading National Park inayotolewa na World Travel Awards mara tano mfululizo kuanzia Mwaka 2019, 2020, 2021, 2022 na 2023.

Tuzo nyingine ni Best Nature Destination World 2023 inayotolewa na Trip Advisor, Tuzo ya ubora wa kimataifa inayotolewa na European Society for Quality Research (ESQR) mara nne mfululizo kuanzia mwaka 2020 (Gold category), 2021 (Platinum category), 2022 (Diamond category) na mara nyingine tena 2023 (Diamond category) na tuzo ya Top Attractions kwa Afrika 2023 iliyotolewa na Trip Advisor kwa Hifadhi za Taifa Serengeti na Tarangire.

Hifadhi ya Taifa Tarangire

Kwa upande wa miradi, Waziri Kairuki anasema TANAPA linatekeleza miradi 108 ya ujirani mwema katika sekta za elimu, afya, usalama, maji na barabara yenye thamani ya Shilingi bil. 40.7 ambapo Shilingi bil. 36.5 ni kupitia ufadhili wa mradi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na Shilingi bil. 4.2 kupitia fedha za miradi ya maendeleo.

“Kati ya miradi hiyo, miradi 75 imekamilika, miradi 10 iko katika hatua za ukamilishaji na miradi 23 ipo katika hatua ya awali ya utekelezaji.

“Aidha, miradi iliyokamilika ni pamoja na ujenzi wa vyumba 44 vya madarasa na ofisi 16 za walimu katika Wilaya za Serengeti, Ngorongoro, Bariadi na Bunda; mabweni manne ya wasichana katika shule za sekondari na msingi zilizopo Wilaya za Mpanda, Same, Mwanga na Serengeti na nyumba 15 zenye uwezo wa kukaa familia 30 za walimu katika Wilaya za Serengeti na Ngorongoro,” anasema Waziri Kairuki katika hotuba yake hiyo.

Kando ya hayo, hotuba ya Waziri Kairuki inazungumzia mipango ya matumizi ya ardhi. Katika hilo, anasema TANAPA limewezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa vijiji 74 vinavyopakana na Hifadhi za Taifa Serengeti ni mipango 37, Ziwa Manyara mipango 25 na Tarangire mipango 12.

Anasema TANAPA limewezesha vikundi 166 vya kiuchumi vya jamii katika Wilaya za Chamwino ni tisa, Iringa 25, Kilolo tisa, Kilombero 56, Kilosa 15, Mvomero 10, Morogoro 26, Meatu vitatu, Itilima tisa na Busega vinne.

Anataja kiwango cha fedha kilichotumika kwa vikundi hivyo ni Shilingi bil 3.22 ili kuvisaidia kuimarika kiuchumi viweze kujiendesha na kupunguza utegemezi wa rasilimali za wanyamapori na misitu.

Anasema TANAPA lilivifikia vikundi 16 katika wilaya tatu; ambazo ni Wilaya za Itilima vikundi tisa, Meatu vikundi vitatu na Busega vinne lililovipatia mizinga ya nyuki 300 pamoja na vifaa vingine vikiwemo mavazi ya kinga 60, vifaa vya ukaguzi kwa Lugha ya Kiingereza vinaitwa bee smoker 75, honey filter 15 na tool hives 60. Pia  vifaa vya uchakataji mazao vinavyofahamika kwa jina la bee pressing machine 15 pamoja na ndoo 300 za kutunzia asali.

Mizinga ya Nyuki

Anazungumzia pia uimarishaji mahusiano kati ya hifadhi na wananchi kuwa TANAPA lilishiriki kikamilifu katika shughuli za uokoaji maafa yaliyotokana na maporomoko ya udongo katika Wilaya ya Hanang.

Anasema TANAPA lilitoa vifaa vya uokozi ikiwemo mitambo (Grader na Excavator) na vikosi vyenye askari 27 na kupitia Msajili wa Hazina liliwasilisha mchango wa Shilingi 10,000,000 ili kusaidia waathirika.

Kuhusu utekelezaji wa shughuli za kila siku za uhifadhi na utalii, Waziri Kairuki anasema TANAPA limeendelea kuandaa na kuhuisha mipango ya ujumla ya usimamizi na uendelezaji (General Management Plans) wa Hifadhi za Taifa.

Anasema kati Julai hadi Aprili, 2024 TANAPA limekamilisha mapitio ya mipango ya ujumla ya usimamizi na uendelezaji wa Hifadhi za Taifa za Ruaha na Nyerere.

Alihitimisha kwa kusema kuwa mapitio ya mpango wa usimamizi na uendelezaji wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi upo katika hatua za ukamilishaji.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya