Monday, December 23, 2024
spot_img

SWEDEN YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA TASNIA YA HABARI

PATTY MAGUBIRA

ARUSHA

SERIKALI ya Sweden imeeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya tasnia ya habari hapa nchini tangu ilipoanza kutoa misaaada na mafunzo kwa vyama vya waandishi wa habari na wanahabari.

Balozi wa Sweden hapa nchini, Charlotta-Ozaki Macias ambaye yuko kwenye ziara ya kikazi akitembelea vyama vya waandishi wa habari Kanda ya Kaskazini, aliyasema hayo jana akiwa katika Ofisi ya Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC).

Alisema Sweden haijutii kuwekeza kwenye tasnia ya habari hapa nchini kutokana na matunda ya kuridhisha ya uwekezaji wake wa takriban muongo mmoja sasa, huku akiweka bayana kuwa kuwekeza kwenye mifumo imara, ukiwemo wa tasnia huru ya habari inachukua muda mrefu.

Sambamba na hilo, Balozi Macias ambaye Serikali yake imekuwa ikitoa mafunzo na misaada mingine kwa vyama  vya waandishi wa habari kupitia Shirikisho la Vyama vya Habari Tanzania (UTPC), aliwakumbusha wanachama na viongozi APC jukumu zito walilonalo kuelekea uchaguzi za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Claud Gwandu akitoa taarifa ya chama hicho kwa Balozi wa Sweden, Charlotta-Ozaki Macias (wa kwanza walioketi kwenye sofa). aliyesisima pembeni ya Gwandu ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya

“Waelimisheni wananchi ili wajiandikishe kwa wingi katika daftari la kudumu la mpiga kura na kutumia fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka,” alisema Balozi Macias.

Aliisifu APC kwa ushirikiano ulionao na serikali akieleza kuwa chama hicho kinashirikiana na Serikali bila kuathiri jukumu la msingi la uandishi wa habari.

Aidha, Balozi Macias alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha ambako Katibu Tawala Msaidizi (Utawala na Rasilimali Watu), David Lyamongi alimueleza kuwa Serikali ya Mkoa na Serikali Kuu zinashirikiana vizuri na vyama hivyo.

“Kwa sasa Serikali inajaribu kutatua baadhi ya changamoto za tasnia ya habari ikiwemo ya waajiri kutowapa mikataba ya ajira waandishi wa habari,” alisema Lyamongi.

Akizungumza katika ofisi hizo, Balozi Macias aliwapongeza waandishi wa habari nchini kwa kuendelea kutekeleza jukumu lao la kuwahabarisha Watanzania licha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali na aliahidi kuwa Serikali ya nchi yake itaendelea kuwa pamoja na waandishi wa habari nyakati zote.

Naye Afisa wa Programu wa Ubalozi wa Sweden, Steven Chimalo ambaye ameambatana na bolozi huyo kwenye ziara yake, alisema anakubaliana na Lyamongi kuhusu ukosefu wa kipato cha uhakika kwa waandishi wa habari jambo linalohatarisha weledi na maadili ya uandishi wa habari.  

“Pamoja na Sheria ya Huduma za Habari kufanya maboresho kadhaa, miongozo ya kisheria bado ina changamoto nyingi kwa tasnia ya habari,” alisema Chimalo.

Rais wa UTPC, Kenneth Simbaya aliwahakikishia wanachama wa APC kuwa umoja wa vyama hivyo unawasiliana na taasisi za Jamii Forum and Nukta Africa ili zitoe mafunzo kwa waandishi wa habari nchini.

Mwenyekiti wa APC, Claud Gwandu alisema chama hicho kinajivunia kuwa na wanachama zaidi ya 60 huku zaidi ya 20 kati yao wakiwa wamejiunga hivi karibuni.

Ziara ya bolizi huyo kwa vyama vya waandishi wa habari Kanda ya Kaskazini inafanyika baada ya kamati ya kutathmini hali ya uchumi katika vyombo vya habari ikitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili waandishi wa habari kuwa ni pamoja na mishahara kidogo, uwekezaji mdogo na zile zitokanazo na kuibuka kwa technolojia mpya.

Kamati hiyo ya watu 10 iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na kuongozwa na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tiddo Mhando kutathimini mwenendo wa vyombo wa habari na uchumi wake, ilieleza katika taarifa yake kuwa asilimia 77 ya waandishi wote nchini hulipwa chini ya Sh. 500,000 kila mmoja kwa mwezi huku wengine wakiambulia Sh. 2,000 kwa habari moja.

Ripoti ya kamati hiyo ilieleza kuwa asilimia 56 ya waandishi wote nchini wanafanya kazi bila mikataba ya ajira kwa hadi miaka sita huku asilimia 38 ya mikataba ya ajira iliyopo ikiwa haina kipengele muhimu cha Bima ya Afya.

Kwamba kutokana na tasnia kudhibitiwa, vyombo vya habari vimejikita kuandika habari za burudani, michezo na uchekeshaji badala ya habari za uchunguzi na ukosoaji.

Taarifa ya kamati ilisema, kudidimia kwa hali ya uchumi wa tasnia ya habari kunatokana na kupungua kwa mapato yatokanayo na matangazo, sera zisizo rafiki za kodi, ukosefu wa weledi katika kusimamia biashara miongoni mwa wamiliki wa vyombo vya habari na ujuzi hafifu miongoni mwa waandishi wa habari unaochagizwa na kuibuka kwa teknolojia mpya.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya