MWANDISHI MAALUMU
KARIKA historia ya maendeleo ya binadamu, afya na lishe zimekuwa nguzo kuu za ustawi wa jamii na taifa. Hali ya mtoto anapokua siyo kielelezo cha familia pekee, bali ni kioo cha afya ya taifa zima. Hii ndiyo sababu mjadala kuhusu utapiamlo na udumavu katika mikoa ya Iringa na Njombe ni mjadala wa maisha na mustakabali wa taifa letu.

Mikoa hii imebarikiwa ardhi yenye rutuba na hali ya hewa inayoruhusu kilimo cha mazao mengi ya chakula. Ni maeneo yanayojulikana kwa kuzalisha mahindi, viazi, mboga, matunda na mazao ya biashara kama chai. Lakini cha kushangaza na kinachoumiza ni kwamba, pamoja na baraka hizo za kiasili, watoto wengi wamedumaa. Swali hili linatufanya kujiuliza: tatizo ni nini hasa?

Takwimu zinaweka wazi ukubwa wa janga. Utafiti wa kitaifa wa lishe wa mwaka 2018 ulionesha kuwa Njombe ilikuwa na viwango vya udumavu vya zaidi ya asilimia 50, huku Iringa ikiwa karibu asilimia 47. Viwango hivi ni vya juu sana ukilinganisha na wastani wa kitaifa uliokuwa karibu asilimia 32.
Hata tafiti za hivi karibuni za SMART zimeendelea kuonyesha kuwa wilaya kama Makete na Njombe Vijijini bado zina viwango vya juu vya watoto waliodumaa. Hali hii inamaanisha kuwa tatizo siyo ukosefu wa chakula, bali ni namna chakula kinavyotumika ndani ya kaya na elimu ya lishe inayotolewa.
Chanzo cha kwanza kinachotajwa mara kwa mara ni elimu duni ya lishe. Wazazi wengi wanajua kulima na kuvuna, lakini hawana uelewa wa kina juu ya aina ya vyakula vinavyohitajika kwa ukuaji wa mtoto. Watoto hukosa protini za kutosha, vitamini na madini muhimu katika miezi ya mwanzo ya maisha, kipindi ambacho ndiyo msingi wa afya yao ya baadaye.
Kuna pia changamoto za kitamaduni na kijamii. Katika baadhi ya kaya, vyakula vyenye virutubisho hubakizwa kwa ajili ya wageni au wanaume pekee, huku watoto na wanawake wakiachwa na mabaki yasiyo na ubora wa lishe. Mila nyingine huzuia watoto kula aina fulani ya vyakula kwa imani za kifamilia, jambo linaloathiri ukuaji wao.

Changamoto nyingine ni mfumo wa kiuchumi wa familia nyingi. Mara nyingi mazao bora zaidi huuzwa sokoni ili kupata kipato cha haraka, huku familia zikibaki kula vyakula visivyo na ubora wa virutubishi. Ni mkakati wa maisha unaoeleweka, lakini matokeo yake ni kuendeleza mzunguko wa udumavu vizazi kwa vizazi.
Serikali, kupitia Wizara ya Afya na mashirika mbalimbali ya maendeleo, imekuwa ikiandaa na kutekeleza programu na mikakati ya kupunguza udumavu. Elimu ya lishe hutolewa kwenye vituo vya afya, bustani kwa ajili ya mazao ambayo huongeza uimara wa afya za watu wazima na watoto katika ngazi za jamii na kaya zimekuwa zikipigiwa chapuo huku pia kampeni za kitaifa kama Mpango wa Taifa wa Lishe (NMNAP) zikiendelea kutekelezwa.
Katika Mkoa wa Njombe, mpango wa Njombe Stunting Reduction Acceleration Response Plan umeanzishwa, ukiwa na malengo ya kupunguza udumavu kutoka karibu asilimia 40 hadi 25 ifikapo 2030. Lakini hata kwa juhudi hizi, ukweli unabaki kuwa bila ushiriki wa jamii wenyewe, mipango hii haiwezi kufanikishwa kikamilifu. Msingi wa mafanikio upo katika kaya na vijiji, siyo ofisi za miji mikubwa pekee. Wananchi ndiyo walengwa na wahusika wakuu wa suluhisho.

Familia zinaweza kuanza na hatua ndogo zenye maana na matokeo makubwa. Kuhakikisha kila familia inakuwa na bustani ya mbogamboga nyumbani, kuhakikisha watoto wanapata chakula chenye mchanganyiko wa virutubisho kila siku na kujifunza mbinu rahisi za kupika zinazohifadhi virutubishi ni hatua zinazoweza kubadili hali.

Shule pia zina nafasi kubwa katika vita hivi. Walimu wanaweza kuwa mabalozi wa lishe bora, wakihamasisha wanafunzi na hata wazazi kupitia elimu ya afya. Shule zenye programu za chakula shuleni zinaweza kutoa mfano bora kwa jamii kwa kuhakikisha watoto wanakula angalau mlo mmoja wenye ubora kila siku.
Viongozi wa dini na mila pia wana nafasi ya kipekee katika hili. Katika jamii ambazo mila au imani zimekuwa kikwazo cha lishe bora, viongozi hawa wanaweza kutumia nafasi zao kuelimisha, kufafanua na kubadilisha mtazamo wa jamii. Ushirikiano wao na wataalamu wa afya unaweza kuondoa imani potofu na kufungua milango ya mabadiliko.
Lishe bora siyo suala la chakula pekee, bali pia la huduma za afya, usafi na upatikanaji na matumizi ya maji safi na salama. Mtoto anayekula vizuri lakini anaugua mara kwa mara kwa magonjwa ya tumbo kutokana na maji machafu bado hatapona udumavu. Hivyo, juhudi za jamii zinapaswa kuunganisha afya, usafi na lishe kama nguzo tatu zinazoshikamana.

Tunapozungumza juu ya udumavu, tusisahau madhara yake kwa taifa. Mtoto aliyedumaa siyo tu mwenye mwili mdogo, bali mara nyingi akili yake pia inakua taratibu. Uwezo wake shuleni hupungua na kadri anavyokua, nguvu yake ya kuchangia kiuchumi hupungua. Taifa lenye watoto wengi waliodumaa linajitengenezea kizazi kisicho na uwezo wa kutosha kushindana kimataifa.
Kwa hiyo, vita dhidi ya udumavu na utapiamlo siyo ya serikali pekee, siyo ya mashirika ya kimataifa pekee, bali ni vita ya kila mmoja wetu. Ni vita ya mama anayeandaa mlo nyumbani, baba anayechagua kuuza au kula mazao yake, walimu shuleni, viongozi wa dini, na kila kijana anayeona mtoto jirani anakua bila lishe bora.
Tusimame pamoja, kwa mshikamano na ushirikiano, tukiamua kwa dhati watoto wa Iringa na Njombe hawatabaki nyuma tena. Tukiamua kutumia ardhi yetu yenye rutuba, maarifa tuliyo nayo na mshikamano wa kijamii tunaweza kuandika upya historia ya lishe katika mikoa hii. Mtoto asiyedumaa leo ni kiongozi imara wa kesho.
