Monday, December 23, 2024
spot_img

MWANZO MPYA WA ANGELLAH KAIRUKI KUELEKEA TANAPA YA MAFANIKIO

MAKALA MAALUMU

ULINZI na uhifadhi wa maliasili, utatuzi wa migogoro ya maeneo baina ya Hifadhi za Taifa na vijiji, uboreshaji maeneo ya malisho ya wanyama, kudhibiti matukio ya mioto kwenye maeneo ya hifadhi, uelimishaji jamii kuhusu shughuli za uhifadhi, kuvutia wawekezaji kuwekeza kwenye huduma za malazi katika maeneo ya hifadhi, kuimarisha miundombinu ya utalii, kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na utalii na uhifadhi ndiyo vipaumbele vya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa sasa.

Vipaumbele hivi vilitangazwa bungeni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki alipokuwa akiwasilisha hotuba ya mpango wa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2024/2025 iliyobeba taswira ya mwanzo mpya wa waziri huyo kuelekea TANAPA iliyoahidiwa kwa Watanzania kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 na uzingatiaji wa Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2025 pamoja na mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/2022 – 2025/2026)

Wabunge wakitekeleza majukumu yao ya kibunge bungeni Dodoma.

Katika hotuba yake hiyo, Waziri Kairuki anasema hadi Aprili, 2024 TANAPA limefanya doria 47,847 huku watuhumiwa 3,323 wa makosa ya ujangili wakikamatwa na silaha za aina mbalimbali.

Anaeleza pia kuhusu mbinu inayotumiwa na askari wa TANAPA kupambana na majangili kuwa ni kanasua mitego ya aina ya nyaya inayotumika kutega wanyamapori; katika hilo TANAPA imetegua mitego 3,103 iliyokuwa imetegwa kwenye Hifadhi za Taifa.

Askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)

Mbinu za kukabiliana na mauaji ya wanyamapori kwa kutegua mitego aina ya nyaya inayotengwa na majangili zimepunguza matukio ya ujangili yakiwemo ya tembo, kutoka wanne waliouawa mwaka 2022 hadi tembo wawili walioripotiwa Aprili, 2024.

Anasema TANAPA limeendelea kutumia teknolojia za kisasa kuimarisha usimamizi na ulinzi wa wanyamapori ikiwemo matumizi ya visukuma mawimbi, doria za kutumia ndege na kuweka alama za masikio kwa faru.

Kwamba, katika mapambano dhidi ya ujangili wa wanyamapori, TANAPA linashirikiana na wananchi na tayari limeanzisha vikundi 17 vya ulinzi shirikishi; katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha vipo vinne, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere vipo vitatu, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi vipo vitatu, Mto Ugalla viwili, Hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa viwili na Kilimanjaro vitatu.

Kuhusu utatuzi wa migogoro ya mipaka, Waziri Kairuki anasema TANAPA  limetatua changamoto ya mpaka kati ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na vijiji saba vilivyopo Wilaya ya Serengeti.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

Anavitaja vijiji hivyo kuwa ni Bisarara, Nyamburi, Bonchugu, Mbalibali, Machochwe, Nyamakendo na Merenga.

Anaeleza pia mpango wa TANAPA kuendelea kuimarisha mipaka ya hifadhi likiwa limeweka vigingi 216 na anataja hifadhi husika na idadi ya vigingi vilivyowekwa, akianza na Hifadhi ya Taifa Serengeti vimewekwa vigingi 184 kwenye maeneo 30 yanayopakana na Vijiji vya Kegonga, Nyandage, Kenyamosabi, Masanga, Karakatonga, Gibaso na Nyabirongo.

Katika Hifadhi ya Taifa Tarangire, anasema vimewekwa vigingi 32 kwenye eneo linalopakana na Vijiji vya Gijedabong na Kimotorok.

Pia TANAPA limefanya uhakiki wa mpaka wa Hifadhi ya Taifa Nyerere kwa upande unaopakana na Mikoa ya Ruvuma, Pwani, Morogoro na Lindi.

Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

Na pia limekamilisha uthamini wa eneo la Ghuba ya Speke lenye ukubwa wa kilomita za mraba 138 ili kuliunganisha na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Akiendelea na hotuba yake, Waziri Kairuki anasema askari wa TANAPA wenye jukumu la kuimarisha uhifadhi na kuboresha maeneo ya malisho ya wanyamapori, wameng’oa mimea vamizi katika eneo lenye ukubwa wa hekta 1,216.

Maeneo yaliyohusika anayataja kuwa ni  Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato hekta 162, Hifadhi ya Taifa ya Katavi hekta 308, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi hekta 110.05, Hifadhi ya Taifa Ruaha hekta 324, Kisiwa cha Rubondo hekta 80, Kisiwa cha Saanane hekta 17, Hifadhi ya Taifa Serengeti hekta 178 na Mto Ugalla hekta 37.1.

Anasena hekta 521,250 zilichomwa kwa mioto ya awali (prescribed burning) kwa utaratibu wa moto mpango (fire management plan) ili kuimarisha nyanda za malisho katika Hifadhi za Taifa za Kitulo, Ziwa Manyara, Milima ya Mahale, Hifadhi ya Taifa Mikumi, Hifadhi ya Taifa Nyerere, Kisiwa cha Rubondo, Saadani, Tarangire na Milima ya Udzungwa.

Matukio ya moto yaliyodhibitiwa na TANAPA anayataja ni 76 katika maeneo ya Hifadhi za Taifa Kilimanjaro, Mikumi, Katavi, Mkomazi, Serengeti, Milima ya Udzungwa na Tarangire.

Kuhusu elimu kwa wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka Hifadhi za Taifa, Waziri Kairuki anasema TANAPA limefanya mikutano 841 iliyohudhuriwa na wananchi 76,289 katika Vijiji 718 vilivyo kwenye wilaya 31 na kwamba wananchi hao walipewa elimu ya namna ya kudhibiti moto, uhifadhi na utunzaji mazingira.

Waziri wa Maliaasili na Utalii, Angellah Kairuki.

Sambamba na hilo, TANAPA lililima kilomita 412.6 za makinga moto katika Hifadhi za Taifa tano anazozitaja kuwa ni Gombe kilomita nane, Mkomazi kilomita 263, Burigi-Chato kilimota sita na Tarangire kilomita 95.5 ili kudhibiti kuenea kwa moto.

Kutoka hapo, Waziri Kairuki anaeleza jitihada zinazofanywa na TANAPA  kuvutia wawekezaji kuwekeza kwenye huduma za malazi na kwamba jitihada hizo zimevuna wawekezaji 27 ambao hivi sasa wanaendelea na ujenzi.

Anasema nyumba za kulala wageni nne, kambi za kudumu 23 zenye vitanda 1,148 zinajengwa katika Hifadhi za Taifa tano ambazo ni Serengeti kukiwa na vitanda 780, Ruaha vitanda 170, Tarangire vitanda 100, Saadani vitanda 50 na Mikumi vitanda 48.

TANAPA linaendelea na ujenzi wa nyumba tatu za kulala wageni za gharama nafuu zenye jumla ya vitanda 178 katika Hifadhi za Taifa Nyerere, Mikumi na Ruaha; pia ujenzi wa hosteli katika Hifadhi za Taifa Ruaha, Mikumi, Saadani na Nyerere pamoja na vituo vitatu vya kutolea taarifa katika Hifadhi za Taifa Serengeti, Ruaha na Mikumi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) George Waitara akipiga mpira kama ishara ya kuzindua ujenzi wa uwanja wa gofu wa kipekee duniani wa Serengeti National Park Golf Course uliopo Fort Ikoma, Serengeti, mkoani Mara.

Kuhusu kuongeza idadi ya watalii na mapato, Waziri Kairuki anasema TANAPA limeibua na kuendeleza mazao mbalimbali ya utalii na anayataja mazao yaliyoibuliwa ni pamoja na utalii wa michezo, ikiwemo tennis kwa kutumia uwanja wa kuhamishika (tennis mobile court) na pia ujenzi wa awamu ya kwanza ya uwanja wa mchezo wa Golf unaotarajiwa kukamilika Disemba, 2024 katika Hifadhi ya Taifa Serengeti unaendelea.  

Anasema TANAPA inajenga daraja la juu linalounganisha vilima na miti (Canopy walkway) katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa ambalo kukamilika kwake kutaongeza uzuri na mvuto wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa.


Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya