RIPOTA MAALUMU
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amefungua shauri Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, chini ya hati ya dharura akiomba nyumba yake iliyokamatwa na mahakama iachiliwe.
Mbowe alifungua shauri hilo hivi karibuni kupitia kwa wakili wake John Mallya, chini ya hati ya dharura, mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mary Mrio.
Nyumba hiyo ilikamatwa kwa amri ya mahakama ili kulipa Sh milioni 62.7 za mishahara ya waandishi wa habari 10 wanaomdai mtoto wake, Dudley Mbowe ambaye ni Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima.
Mbowe kafungua shauri dhidi ya waandishi wa habari Maregesi Paul, Fidelis Felix, Christina Mwakangale, Janeth Josiah, Exuperius Kachenje, Hellen Sisya, Kulwa Mzee, Nora Damian, Makuburi Ally, Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima na Kampuni ya Udalali ya JJ Auctioneers & Debt Collectors.
Wakili Mallya alidai wajibu maombi tayari wamepewa madai yao pamoja na hati ya kiapo iliyoapwa na Mbowe, Februari 26, mwaka huu.
“Mheshimiwa wajibu maombi tumeshawapa nakala hivi karibuni tusikilize kama wamekuja na majibu,” alidai Mallya mahakamani hapo.
Akijibu hoja hizo, mmoja wa wajibu maombi, Kulwa Mzee, alidai ni kweli wamepokea nyaraka hizo zikiwa zimeambatanishwa na hati ya kiapo iliyoapwa na Mbowe akiomba nyumba iachiliwe na Mahakama itoe amri wajibu maombi wamlipe gharama kutokana na utekelezaji wa amri hiyo ya Mahakama.
“Mheshimiwa tumepitia nyaraka, wenzetu wametupa siku 15 tujibu, tunaihakikishia Mahakama kwamba tutajibu ndani ya muda tuliopewa,” alidai Mzee.
Wakili Mallya aliomba kujibu hoja hiyo, alidai shauri lao wameliwasilisha chini ya hati ya dharura, maombi yao ni kuiondoa nyumba hiyo kwani tayari ilishabandikwa matangazo kwa ajili ya kupigwa mnada.
Alidai ikiendelea kuwa kama ilivyo inaweza kupigwa mnada kwa sababu suala hilo lina muda wa utekelezaji.

Maregesi Paul
Akijibu, Mzee alidai ni kweli maombi yako katika hati ya dharura lakini lazima yasomwe vizuri ili wajibu kwa kuwasilisha hati ya kiapo kinzani kwa sababu katika maombi hayo kuna suala la kumlipa mwombaji gharama.
Aliomba kuwa kama siku 15 ni nyingi watajibu ndani ya siku saba. Mahakama ilikubali majibu yawasilishwe mapema na shauri hilo litasikilizwa Machi 12, mwaka huu.
Mbowe katika madai yake anadai nyumba iliyokamatwa si mali ya Dudley na kwa kuthibitisha hilo aliambatanisha hati ya nyumba hiyo yenye jina la Freeman Mbowe.
Mahakama hiyo pia imepanga kuendelea na shauri la madai ya waandishi hao kwa Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley, Machi 12, mwaka huu.
Februari 13, mwaka huu Mahakama ilikubali maombi ya wadai na kumteua dalali wa Mahakama kukamata nyumba kwa ajili ya kuipiga mnada.
Februari 28 mwaka huu, dalali wa Mahakama, Jesca Massawe alifanikiwa kubandika matangazo ya kukamata nyumba hiyo tayari kupigwa mnada kufidia deni la malimbikizo ya mishahara ya waandishi wa habari.
Shauri hilo lililomfikisha Mbowe mahakamani ni namba 28461 la mwaka 2023, wadai wakiwa Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.
Baada ya mdaiwa kukaidi kulipa, wadai walikubaliana njia sahihi ni kukamata nyumba yake iliyopo Mtaa wa Feza, Mikocheni B, barabara ya Chipaka na Mahakama ilikubali.
Maregesi na wenzake walipata tuzo ya mahakama Julai 17, 2023 mbele ya Msuluhishi wa CMA Ilala, Bonasia Mollel.
Katika shauri hilo, madai ya awali ya Maregesi na wenzake yalikuwa Sh. milioni 114 lakini baada ya kuketi kwenye meza ya majadiliano, kiwango hicho kilishuka na kufikia Sh milioni 62.7.
Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30 mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni mwa Februari, mwaka huu, lakini hakulipa.