RIPOTA PANORAMA
TAASISI ya Frankfurt Zoological Society (FZS) iliyonunua gari lililotolewa msaada kwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa ajili ya shughuli za uhifadhi, imesema Serikali ndiyo yenye mamlaka ya kuzungumzia skandali ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamedi Mchengerwa ya kutokomea na gari la mradi wa uhifadhi kwa zaidi ya miezi mitatu.
Akizungumza leo asubuhi na Tanzania PANORAMA Blog kwa simu akiwa ofisini kwake mkoani Arusha, Mkurugenzi Mkazi wa Tanzania Frankfurt Zoological Society, Dk. Ezekiel Dembe amesema chombo chake ni Shirika Lisilokuwa na Kiserikali (NGO), ambalo lilipewa kazi na Serikali ya Ujerumani kununua gari hilo kisha kulikabidhi lakini haihusiki kufuatilia shughuli zake.
Dk. Dembe amesema baada ya kununua gari hilo walimkabidhi Balozi wa Ujerumani hapa nchini ambaye alimkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye naye alimkabidhi Waziri wa Maliasili na Utalii na yeye alimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya TANAPA.
“Yale magari tulitoa sisi ndiyo lakini ni mradi ambao, ni kati ya Serikali ya Tanzania na Ujerumani, wakapitisha hela kwetu kwamba tuwasaidie kununua kwa sababu Serikali ya Ujerumani walisema hawawezi wakaweka TANAPA kwa sababu hizo hela na wao kama kawaida wanajua ………
“Kwa hiyo wakapitia kwetu sisi tukawanunulia hayo magari, tukawakabidhi, tukamkabidhi Balozi, Balozi akamkabidhi Waziri Mkuu, Waziri Mkuu akamkabidhi Waziri, Waziri amkakabidhi Mwenyekiti wa Bodi TANAPA, ndiyo yakawa yameishaenda.
“Sasa magari yakishaenda, mara nyingi, maana siyo hayo tu ni mengi tu tumeishatoa, taasisi hii imekuwepo kwa zaidi ya miaka 60, magari yanatolewa, wanapelekewa wanatumia. Makubaliano yaliyopo ni miradi hiyo…… ndiyo unakuta yanakuwa DFP lakini kwa haya yaliyokuja kwa sababu yaliletwa TANAPA kwa sababu ya COVID ambayo iliua utalii, walisaidiwa hayo magari ndiyo maana yameandikwa namba za Jeshi Usu.
“Sasa magari yale yakishaandikwa vile sisi hatuhusiki nayo tena na ndiyo maana yanakabidhiwa rasmi. Na ndiyo maana tunasita, maana sisi tukisema jambo na sisi tunafanya kazi hapa kwa makubaliano na Wizara ya Maliasili na Utalii….,” alisema Dk Dembe na kuongeza kuwa.
“Inawezekana viongozi wakatumia lakini lazima yanarudi, hayaondoki na hata kama wanafanya hivyo ni arrangement yao sisi hatusemagi neno na ndiyo maana tunasita tukisema neno lolote…. Sijui kama unanielewa,’ alisema Dk Dembe.
Akizungumzia kuhusu Waziri Mchengerwa kutokomea na gari hilo kwa zaidi ya miezi mitatu, Dk Dembe alisema “… sisi kwa kweli hatuna nia yoyote, wala hatufichi jambo lolote wala nini,……. Ukweli ni kwamba it was wrong, hilo tukubaliane kwamba it was wrong, lakini wanaotakiwa kulifafanua vizuri ni wenzetu …..ambao ndiyo magari tuliwakabidhi,” alisema Dk. Dembe.
Akiendelea, Dk. Dembe alisema kama kuna mtu wa kulalamika kuhusu magari hayo ni Serikali ya Ujerumani na kwamba watataka kujua ni kwanini jambo kama hilo limetokea. Jitihada za Tanzania PANORAMA Blog kumpata Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania ili kupata kauli yake kuhusu suala hilo zinaendelea.
Kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, Waziri Mchengerwa ametokomea na gari la kisasa la mradi wa uhifadhi, aina ya Nissan Patrol – Wagon, lenye namba za usajili 02 JU 0480 lililotolewa msaada na Taasisi ya Frankfurt Zoological Society (FZS) kwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na kila alipoulizwa hakutoa jibu lolote.
Waziri Mchengerwa alipewa gari hilo na TANAPA wakati wa ziara yake ya kikazi kwenye Hifadhi za Taifa ya Juni 18, mwaka huu lakini alipomaliza alitokomea nalo na hata alipohamishwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda TAMISEMI, hakulirudisha kwenye mradi liliokusudiwa.
Msemaji wa Wizara ya Maliasili ba Utalii, John Mapepele ambaye awali alithibitisha Waziri Mchengerwa kutokomea na gari hilo la msaada na kwamba sasa anapaswa kulirudisha, leo ametoa kanusho kuhusu alichokithibitisha akisema ni uzushi na uongo.
Mapepele alithibitisha Waziri Mchengerwa kutokomea na gari hilo, alikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa siyo Waziri Mchengerwa pekee, bali makatibu wakuu na viongozi wengine wa Serikali wanapoteuliwa na kukuta magari waliyopangiwa siyo mazuri huwa wanachukua magari mazuri kwenye taasisi.
Alisema wapo viongozi wa Serikali ambao wanapoteuliwa huwa wanakuta ofisi zao hazina magari hivyo kulazimika kuchukua ya taasisi huku akalitaja kosa la Waziri Mchengerwa kuwa ni kuondoka na gari hilo baada ya kuhamishwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda TAMISEMI.
Kanusho la Mapepele linaeleza kuwa gari alilotokomea nalo Waziri Mchengerwa awali liliazimwa wizarani kwa utaratibu wa kawaida na kwa barua yenye kumbukumbu namba A. B 307/402/01/38 limeombwa kutumika kwa muda Ofisi ya Rais TAMISEMI na kufuata taratibu zote za Serikali huku akitishia kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa aliowaita wahusika.
Msemaji huyo wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mapepele katika kanusho lake haufahamishi umma, gari lililochukuliwa Juni 18, 2023 na Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye alihamishiwa TAMISEMI Agosti 30, 2023, mpaka sasa Septemba 25, 2023 bado analo; TAMISEMI ililiomba kabla ya waziri kuhamishwa au baada, sababu za TAMISEMI kuomba gari hilo ni zipi na iwapo Serikali haina gari kwa ajili ya Waziri wa TAMISEMI.