Tuesday, August 26, 2025
spot_img

MADUDU UVINZA

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

Uvinza, Kigoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameigiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rishwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma, kuwachunguza viongozi wa Halmashauri ya Uvinza na kubainisha mkwamo wa miradi ya maendeleo.

Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa wa Kigoma,   Steven Mafiga kuwachunguza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Zainab Mbunda na Mweka Hazina, Majjid Mabanga ili kubaini ni kwa nini miradi haiendi wakati fedha zilishatolewa.

Agizo hilo alilitoa Alhamisi, Septemba 21, 2023) wakati akizungumza na watumishi na wananchi waliohudhuria uwekaji wa jiwe la msingi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, lililoko Lugufu, Uvinza, mkoani Kigoma.

“Kamanda wa TAKUKURU Mkoa kamilisha hiyo kazi kwa haraka sana. Rais wetu analeta fedha nyingi sana lakini kuna watu hawafanyi maamuzi. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Mweka Hazina wakae pembeni kupisha uchunguzi,” alisema.

Agizo hilo la Waziri Mkuu alilitoa baada ya kubaini kuwa fedha za miradi ya ujenzi wa hospitali ya wilaya, vituo vya afya vya Rukoma na Sunuka na zahanati za Mgambo na Kajeje zilizotumwa tangu mwaka 2021/2022, zinadaiwa kuwepo kwenye akaunti wakati majengo husika hayajakamilika na taarifa inayotolewa inasema ujenzi uko kwenye hatua ya ukamilishaji.

“Kwa nini lugha ya ukamilishaji hapa Uvinza imeshamiri? Fedha za miradi zikiletwa ziende kwenye kazi iliyokusudiwa. Sasa hapa, Mkurugenzi anasema fedha zipo, Mweka Hazina anasema zimeisha, Mhandisi aliandika dokezo la kuomba vifaa, mtu wa manunuzi anasema hajalipata. Fedha zipo na kazi haziendi. Nimewaweka pembeni kwa sababu nimeona usimamizi ni mbovu.

“Leo hii tukitoka Nguruka, Kamanda wa TAKUKURU ingia kazini, angalia hizo fedha ziko kwenye akaunti zipi, angalia kuna shilingi ngapi na zilikuwa zimepangwa kufanya shughuli gani,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kabla ya kuweka jiwe la msingi wa jengo la ofisi ya halmashauri hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa alikagua hospitali ya wilaya hiyo na kubaini majengo kadhaa hayajakamilika licha ya kuwa fedha zilitolewa tangu Mei, 2021.

Pia alikuta vifaa tiba vingi vikiwa kwenye chumba ambacho hakina milango wala vipoza hewa (Air conditioner) huku vikiwa vimejaa vumbi.

“Ni kwa nini vifaa hivi kwa kielektroniki tena vya gharama kubwa vimeachwa tu hapa, tena vinapigwa na vumbi? Hamuoni huruma kwa fedha za Serikali?” alihoji.

Waziri Mkuu alisema ametembelea mikoa mbalimbali hapa nchini na kuweka mawe ya msingi ama kuzindua majengo ya wagonjwa wa dharura (EMD) lakini haelewi ni kwa nini majengo ya Uvinza hadi leo hayajakamilika.

“Kibondo na Kasulu wenzenu wamekamilisha majengo yao, iweje hapa Uvinza bado tu?” alihoji Waziri Mkuu.

Akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa hospitali ya wilaya, mkuu wa kituo wa hospitali hiyo, Dk. David Patrick alisema mwaka 2019 walipokea Sh. bilioni 1.5 za ujenzi wa majengo saba, kisha wakapokea Sh. milioni 300 za njia ya watembea kwa miguu.

“Mei, 2021 tulipokea shilingi milioni 500 za wodi tatu na Machi, 2022 tulipokea shilingi milioni 390 za EMD na nyumba ya watumishi. Pia tulipokea shilingi milioni 523 za vifaa tiba.

“Halmashauri ya Wilaya Uvinza ilipokea fedha kiasi cha Sh. bilioni moja na milioni mia tano, mwaka 2019 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba ya awali ambayo ni jengo la mionzi, wodi ya wazazi, maabara, wagonjwa wa nje, utawala, madawa, jengo la kufulia. Utekelezaji wa mradi wa Hospitali ya Wilaya ulianza tarehe 10 Januari, 2019,” alisema Dk. Patrick.

Mapema, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulia Afya, Dk. Festo Dugange alisema Serikali ilitoa Sh. bilioni 1.9, kisha ikatoa Sh. milioni 170 na Julai, mwaka huu imetoa milioni 750 kwa ajili ya ujenzi jengo la halmashauri ambalo hadi sasa lilipaswa kuwa limekamilika.

“Nawapa muda hadi tarehe 30 Oktoba, 2023 liwe limekamilika na limeanza kutoa huduma,” alisema.

Kuhusu Hospitali ya Wilaya ya Uvinza, Dk. Dugange alisema fedha zilianza kutumwa mwaka wa fedha 2019/2020 na hadi sasa Sh. bilioni 3.4 zimeshapokelewa.

“Julai 2021 tulikuja kukagua na kuelezwa kuwa majengo yangekamilika ifikapo Desemba, 2021. Shilingi milioni 300 za EMD zilitumwa lakini bado jengo hilo halikamilika,” alisema.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya