RIPOTA PANORAMA
MTU anayedemka ngomani bila kufuata mdundo wa ngoma, huhambukwa tu kwa sababu hajioni kama anakosea. Amesema Rais Samia Saluhu Hassan jana.
Alikuwa akizungumza wakati akifungua mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa unaofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais Samia kufanyia kazi mambo yanayohusu demokrasia mambo mengi.
“Hata tunapokuwa kwenye ngoma, kama unacheza huendi na mdundo. Wa nje ndiye anakuona wewe unayedemka humo ndani ya ngoma hujioni kwamba unakosea steps au huendi na mdundo, hujioni. Umo tu unahambukwa,” alisema Rais Samia.
Akifafanua kauli yake hiyo, Rais Samia alisema hakuna jambo lisilokuwa na kasoro ikiwermo uendeshaji wa shughuli za vyama vya upinzani na hata serikalini na alishauri njia nzuri ya kuepukana na kasoro hizo ni kujadiliana na kuelekezana.
“Katika dunia hii hakuna jambo lisilokuwa na kasoro. Hakuna popote ulimwenguni, kila kitu kina kasoro zake. Katika kuendesha Serikali kuna kasoro, kwenye vyama vyenu vya siasa kuna kasoro tena kubwa tunawasikia mnalumbana huko.
“Lakini jambo la busara ni kuondoa kasoro kwa kuelimishana, kuelekezana na kujadiliana. Tukikaa kuelimishana, kuelekezana na kujadiliana tutakuwa tunaondosha kasoro zetu.
“Hivyo nitoe rai kwa vyama vya siasa na taasisi za kiraia kwamba kunapokuwa na kasoro zozote katika mifumo yetu, au kuna mambo fulani hayaendi sawa, jambo la busara ni kuelezana, kujadiliana kama tutakubaliana ama tutatoka bila kukubaliana ni vyema kuwa na msimamo wa kuiwezesha demokrasia yetu kushamiri,” alisema.
Akiendelea kuhusu hilo, Rais Samia alisema haiwezekani watu wote wakazungumza na kukubaliana katika kila jambo lakini inapotokea kutokubaliana, demokarasia ichukue mkondo wake kwa kuwapa wengi na kuheshimu mawazo ya wachache.
“Sasa unapotoka hujakubaliana na wenzio basi tutoke na msimamo kwamba demokrasia iendelee kushamiri. Usitoke kwamba mimi sijaridhika naenda kuvuruga kila kitu cha nchi nzima kwa sababu wewe mmoja hujaridhika; nyie wawili hamjaridhika. Hatuendi hivyo.
“Na ndiyo maana kuna ule msemo wanasema wengi wape lakini wachache waheshimiwe. Tunapotoka hatujakubaliana, kama wengi wamekubali twende na makubaliano ya wengi.
“Lakini wachache ambao hawakukubali, tuheshimu mawazo yao, tuyafanyie kazi tuone tunakwendaje ndipo tutakaposhamirisha au kunawirisha demokrasia ndani ya nchi yetu,” alisema Rais Samia.