RIPOTA PANORAMA
MWENYEKITI Mtendaji wa Kampuni za Taifa Group, Rostam Aziz ameeleza kukerwa na tabia ya mtu anayejiita Kigogo kufuatilia kazi za kampuni yake ya Taifa Gesi.
Ameeleza hayo katika taarifa rasmi iliyotolewa na ofisi yake leo, Mei 5, 2023 kuwa mwenendo wa mtu huyo kufuatilia kazi za kampuni yake ya Taifa Gesi, akiipongeza kwa utendaji kazi wake kusitafasiliwe kuwa mtu huyo anafahamika kwenye kampuni hiyo na au inamtuma.
Rostam ambaye ni mfanyabiashara mwenye ukwasi mkubwa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na pia mwanasiasa aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwa ni pamoja na kuwa wa Igunga, amesema umma ufahamu kwamba hana uhusiano wowote na Kigogo na hapendi kuhusishwa naye kwa namna yoyote.
“Ndugu Rostam hakubaliani na tuhuma kadha wa kadha zisizo na msingi wala ukweli ambazo huyu bwana amekuwa akizielekeza kwake binafsi na wakati mwingine kwa viongozi wa Serikali na watu wengine kadhaa.
“Ikumbukwe kwamba, wakati fulani mtu huyo huyo alipata kumjeruhi ndugu Rostam na mke wake wakati ule wa mlipuko wa COVID 19 kwa kuandika taarifa ambazo baadaye zilikuja kubainika hazikuwa na ukweli wowote,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Anaandika zaidi kuwa anawasihi watanzania wanaotumia na kufuatilia mitandao kuzingatia misingi ya utu, uwajibikaji na kuwa makini na yale wanayoyaandika au yale yanayoandikwa na kupuuza uzushi na uongo unaoandikwa mitandaoni.
“Mara kadhaa kumekuwa na taarifa katika mitandao za kuua na kufufua watu zinazotengezwa mithili ya hadithi za kufikirika za Alfu Lela Ulela na wakati mwingine kutuhumu watu kwa wizi huku wengine wakitengezwa waonekane ni Malaika. Haya ni mambo ya kukemea kwa nguvu zetu zote,” inasomeka taarifa ya Rostam.
Tamko hilo la Rostam linakuja siku chache baada ya kuibuka tetesi zilizodai kuwa mtu anayejiita Kigogo alisafiri kutoka nchi ya ughaibuni anakoishi na kukutana na baadhi ya watu wakubwa wanaodaiwa kumpa maelekezo mahususi ya kuelekea uchaguzi mkuu ujao.






