PAPA BENEDICTO XVI KUTOKA 1927 HADI 2022

Date:

Share post:

MASHIRIKA YA HABARI

VATICAN

Kardinali Joseph Aloisius Ratzinger ambaye ndiye Papa Benedicto wa XVI, ameumaliza mwendo, amepigana vita vilivyo vizuri, imani ameilinda.

Papa Mstaafu Benedicto XVI aliyekuwa na umri wa miaka 95 alifariki dunia Disemba 31, 2022 majira ya saa 3.34 asubuhi katika Hosteli ya Mater Ecclesiae iliyoko kwenye Bustani za Vatican ambako ndiko alikuwa na makazi yake tangu mwaka 2013 alipong’atuka kutoka kwenye kiti cha upapa kwa sababu za umri wake kuwa mkubwa.

Historia ya maisha yake inaonyesha kuwa, Joseph Aloisius Ratzinger, alizaliwa Aprili 16, 1927 huko Markti nchini Ujerumani na alisoma masomo ya majiundo yake ya kikasisi kabla ya kupewa daraja takatifu ya upadre Juni 29, 1951 wakati wa sherehe ya watakatifu Petro na Paulo, mitume wanaotambuliwa na Kanisa Katoliki kama miamba ya imani.

Akiwa Padre, vipaji vyake yalianza kung’ara na kuwa kati ya wanataalimungu mahiri waliojipambanua katika miaka 1950 ndani na nje ya Ujerumani; akifundisha katika vyuo vikuu kadhaa vya taalimungu nchini Ujerumani.

Mei 28, 1977 Papa wa wakati huo, Mtakatifu Paulo VI alimteua kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Munich na Freising na mwezi mmoja baadaye, Juni 27, 1977 alimteua kuwa Kardinali. Uteuzi wa Ratzinger kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Munich na Freising uliwashangaza wengi kwa ssbabu hakuwa na uzoefu wa kutosha katika shughuli za kichungaji kama Askofu lakini alihudumu kwa mafanikio nafasi hiyo kuanzia 1977 hadi 1982.

Kardinali Ratzinger alichaguliwa kuwa Papa wa 265, Aprili 19, 2005 akiwa na umri wa miaka 78 na kuhudumu katika nafasi hiyo ya juu zaidi ya uongozi wa Kanisa Katoliki kwa muda wa miaka nane hadi alipojiuzulu Februari 11, 2013 ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine kuliongoza Kanisa Katoliki na mrithi wake aliyechaguliwa ni Papa Francis.

Papa Mstaafu Benedicto wa XVI akiwa na Papa Francis siku alipong’atuka madarakani

Nyadhifa alizoshika katika Kanisa Katoliki kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 2005 ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Rais wa Tume ya Taalimungu Kimataifa na Tume ya Biblia Kimataifa pamoja na Dekano wa Baraza la Makardinali.

Hotuba yake ya kwanza akiwa Papa baada ya kifo cha Papa Yohane Paulo II aliyekuwa maarufu sana duniani wakati huo, alisema Makardinali wamemchagua yeye mtu wa kawaida na mfanyakazi katika shamba la bwana kuwa Papa lakini Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anatambua jinsi ya kuendeleza kazi yake hata kwa kutumia vyombo dhaifu kama yeye.

Akiwa katika kilele cha uongozi wa Kanisa Katoliki baada ya safari yake ndefu ya ukasisi na uaskofu, Papa Benedikto XVI aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kusimikwa rasmi kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Aprili 24, 2005 na ujumbe wake alioutoa siku hiyo ulisema vishawishi vikuu vinavyowaandama wanadamu katika ulimwengu mamboleo ni uchu wa fedha na mali, madaraka na elimu; mambo yanayoendelea kusababisha ukinzani na mipasuko katika maisha ya wanadamu.

Katika kipindi cha uongozi wake katika Kanisa Katoliki, Papa Benedikto XVI alianzisha mchakato wa mageuzi kwenye Sekretarieti Kuu ya Vatican huku akikumbana na ‘vizingiti’ katika maisha na utume wake na pia katika kipindi chake cha miaka nane, viongozi wa Kanisa Katoliki kutoka Bara la Afrika walianza kupata nafasi za uongozi wa juu kama wakuu wa Mabaraza ya Kipapa na wengine kutumwa sehemu mbalimbali duniani kama mabalozi wa Vatican.

Upapa wake alikazia zaidi imani, matumaini na mapendo kama mambo msingi ambayo yangewawezesha waamini kujenga na kuimarisha uhusiano na ufungamano wao na Yesu Kristo.

Papa Benedikto XVI

Akiwa madarakani, Papa Benedikto wa XVI aliandika nyaraka za kitume ikiwemo inayojulikana kwa Lugha ya Kirumi, Deus Caritas Est, yaani Mungu ni upendo. Nyaraka zingine alizoandika ni Spe salvi yaani matumaini yanayookoa, Caritas in veritate yaani ukweli katika upendo na wosia wa kitume ambao hakumaliza kuuandika kama hitimisho la maadhimisho ya mwaka wa imani ambao kwa Lugha ya Kirumi unajulikana kama Lumen fidei, yaani mwanga wa imani.

Ni katika kipindi chake cha upapa, baada ya maadhimisho ya Sinodi mbalimbali, Papa Benedicto wa XVI aliandika wosia zifuatazo; Verbum Domini yaani Neno la Mungu, Ecclesia in Medio Oriente yaani Kanisa Mashariki ya Kati, Sacramentum Caritatis yaani Sakramenti ya upendo na Africae munus yaani dhamana ya Afrika.

Pia Katekisimu ya Kanisa Katoliki: muhtasari wa imani, Sakramenti za Kanisa, maisha adili na maisha ya sala na maadhimisho ya mwaka wa Imani.

Papa Benedicto wa XVI aliliangalia Bara la Afrika kwa jicho la karibu na miongon mwa maamuzi yake kuhusu Bara la Afrika ni kuridhia uamuzi ya Papa Yohane Paulo II wa kuadhimisha awamu ya pili ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki barani Afrika, iliyofanyika Vatican kuanzia Oktoba 4 hadi 25, 2009. Uamuzi huo ulitangazwa na Papa Yohane Paulo II, Novemba 13, 2004 lakini alifariki dunia kabla ya kuutekeleza.  

Papa Benedicto XVI alifanya hija ya kitume katika Bara la Afrika kuanzia Machi 17 hadi 23, 2009 kwa kuzuru nchi za Angola na Cameroon na kuzindua hati ya kutendea kazi na Novemba 9, 2011 aliwasilisha wosia wa kitume, Africae munus yaani Dhamana ya Afrika huko Benin kwa heshima ya Kardinali Bernardin Gantin aliyeishi na kufanya naye kazi kwa miaka mingi mjini Roma.

Papa Mstaafu Benedikto wa XVI akiwa na baadhi ya Makardinali

Katika wosia wake wa kitume kwa Bara la Afrika unaotambulika kama Dhamana ya Afrika, Papa Benedicto anawausia waafrika kuwa; Bara la Afrika ni mahali pa kufanyia kazi kwa ajili ya upatanisho, haki na amani, kufanya toba, wongofu wa ndani, kwa kujali utu na heshima na haki msingi za binadamu.

Ujumbe wake kwa waafika katika wosia huo unaeleza kuwa familia ya Mungu barani Afrika haina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kuheshimu na kutunza mazingira na kanisa barani Afrika lisaidie juhudi za utawala bora kwa kuheshimu utawala wa sheria, demokrasia shirikishi; uhuru na haki msingi za binadamu.

Kwamba hiyo ni changamoto na mwaliko wa kuonesha mshikamano wa hali na mali kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalumu. Utu, heshima na haki zao msingi ni mambo ya kuzingatiwa na wote na alilihamasisha kanisa barani Afrika kujenga na kudumisha utandawazi wa upendo na mshikamano.

Kwenye sehemu ya pili ya wosia wake huo wa kitume, Africae munus anakazia umuhimu wa kushirikishana karama akiwahimiza zaidi maaskofu kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na familia ya Mungu ili kuendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia habari njema.

Alilihimiza Bara la Afrika kuwekeza katika sekta ya elimu, huduma ya afya na katika teknolojia na ulimwengu wa mawasiliano ya jamii na zaidi kwamba kanisa liendelee kuwafundisha waamini umuhimu wa neno la Mungu na ushiriki makini katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa hususan Ekaristi Takatifu kuwa chanzo na utimilifu wa maisha na utume wa kanisa.

Alihitimisha wosia wake kwa kuwataka waafrika kujipa moyo, kuinuka na kuanza safari ya haki, amani na upatanisho kwani wao ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu.

Februari 11, 2013 ambayo kwa wakatoliki ni siku ya kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes (1858) na kumbukumbu ya Mkataba wa Lateran (1929), Papa Benedicto XVI aliamua kwa hiari yake mwenyewe kung’atuka kutoka kwenye kiti cha upapa kutokana na uzee pamoja na kuanza kuzorota kwa afya yake ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine kuendeleza dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

About The Author

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

USIYOYAJUA KUHUSU KOCHA ALIYEANDIKA HISTORIA BUNDESLIGA

MUNICH, Ujerumani JINA la Marie-Louise Eta limeandika historia katika soka la Ujerumani baada ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa...

BURNA BOY HATAKI MAZOEA, ‘BIFU’ KWAKE KAWAIDA TU

HIVI karibuni, supastaa wa muziki wa Afrobeat, Burna Boy, aliingia kwenye mikono ya Chama cha 'Ma-dj' nchini Nigeria,...

BURKINA FASO IKO HOI AU HAI CHINI YA KAPTENI TRAORE?

HATUA ya kutangaza kuwa raia wake waaitarajie demokrasia imeibua maswali mengi juu ya uongozi wa Kapteni Ibrahim Traore...

SIMU YAKO CHANZO CHA UGONJWA WA MOYO, SARATANI?

UKWELI ulio wazi ni kwamba matumizi ya simu za mkononi yameongezeka kwa kasi duniani, Tanzania ikiwa na 'laini'...