Monday, December 23, 2024
spot_img

KESHO TUTACHEKWA PAMOJA NA KIKWETE

KILA ninaipoitazama Tanzania ya kesho ninawaona watoto wa watoto wetu wakitucheka kwa kushindwa kuiishi misingi ya utawala bora, kutofuata sheria za nchi, wanasiasa kuendekeza ulafi wa madaraka walioujenga katika misingi ya chuki, fitna, majungu na kuisigina Katiba ya nchi.
Watoto wa watoto wetu ninaowatazama katika safu hii kwa jicho la kichokonozi, ninawaona wakihangaika kuperuzi nyaraka mbalimbali zilizotumiwa na watawala wetu wa sasa kuliongoza taifa letu ili ziwe msaada kwao katika kuchukua uamuzi lakini hawaoni inayowafaa.
Ni chache sana zinasomeka bila kuacha maswali lakini hata hizo wanalazimika kuzihariri kwanza.
Wakiwa katika hali hii, ninawaona watoto hawa wakicheka kwa dharau na mshangao huku wakijiuliza ni aina gani ya watu walioishi katika taifa hili kabla yao! Yaani nyakati zetu za sasa. Watu ambao kwa kiasi kikubwa historia ya wakati huo itakuwa ikiwakumbuka kwa mabaya. 
Watoto hawa nawaona wakisoma kwa mshangao historia ya utendaji kazi wa Serikali wa Awamu ya Nne, jinsi ilivyokuwa ikichukua uamuzi hata katika mambo ambayo isiyoyaamini kwa sababu tu ya kushinikizwa
Watoto hawa nawaona wakiwa wamekodoa macho kwenye vitabu chakavu vya historia ya Bunge na wabunge na kushangaa aina ya wabunge waliopata kuwapo Tanzania wakiwemo wenye elimu ya kubabaisha na mabingwa wa mipasho.
Wote wanashangaa jinsi baba na babu zao tulivyoshindwa kuyaangalia kwa uzito unaostahili  mambo yenye athari mbaya kwa taifa.
Mbali ya watoto hao, wajukuu wa wajukuu wa wajukuu zetu ambao wakati huo watakuwa wanafunzi wa sekondari na vyuo, hawa nawaona tofauti kidogo na baba na mama zao.
Nawaona wakiitazama Tanzania ya sasa kama taifa lililojaaliwa baadhi ya watu wenye akili lakini likakosa bahati ya kupata viongozi bora.
Msingi wa imani hii kwa wajukuu hawa utakuwa maandishi ya waandishi wenye fikra pevu na wachambuzi wa masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa, elimu na hata kiuchumi ambayo watakapokuwa yakiwasoma watakuwa wakitoa hukumu dhidi yetu kulingana na maandishi hayo hayo, maneno na matendo yetu ya sasa.
Wakiongozwa na maandishi hayo ya kichokonozi, wajukuu zetu katika ulimwengu wao wa wakati huo watakaokuwa wakiishi na ambao ninautizama na kuuona utakuwa bora mno kuliko huu wa sasa. Wakiwa wanasoma, watakuwa wanasema:
“Hakika! Tanzania ya wakati ule, miaka mingi iliyopita, baba wa babu zetu waliishi na Mchokonozi aliyekuwa na fikra pevu. Walisoma maandishi ya kufikirisha ya rafiki huyo mwema wa watawala aliyekuwa akizungumza nao kwa upendo wa kichokonozi kuhusu mwenendo wao wa kiutawala lakini kwa sababu ya kiburi na ubinafsi, hawakumsikiliza.
“Kutosikiliza kwao kulisababisha anguko lao lililozaa vuguvugu la mapinduzi ya uongozi wa kufikirika ambao baadaye ulizaa uongozi wa kizazi kipya.”
Na pengine katika mtizamo huu uliojificha katika ndoto halisi, watakuwa wakisema: “Nchi yetu Tanzania, miaka mingi iliyopita ilikuwa sawa na paradiso lakini kwa sababu ya ujinga wa watawala waliigeuza ikawa sawa na kuzimu. Wanastahili laana kwa uongozi wao wa kipuuzi, uliojaa tamaa, ubinafsi na kila aina ya mbwembwe za kijuha.”
Huku wakigonga vingaja vya mikono yao na kucheka vicheko vyepesi wakiwa wamezama katika kusoma historia ya kale itakayokuwa imetunzwa katika vitabu chakavu vya historia ya mapinduzi mepesi ya uongozi ninayoyafikiria kutokea hivi karibuni, kwa sauti za kunong’ona watakuwa wakisemezana: “Tuandike script za igizo la Escrow!”
Ndani ya vitabu hivyo chakavu wajukuu zetu watasoma jinsi wachambuzi wa mambo ya siasa walivyoandika maandishi ya kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kuona jinsi kilivyoshindwa kuongoza, kilivyogeuka kutoka katika misingi yake ya awali ya chama cha wakulima na wafanyakazi na kuwa chama cha wafanyabiashara walafi na matapeli. Kwa sababu hata wakati huo watakuwepo matapeli na vijana hao watakuwa wanacheka sana wakiwalinganisha na wa CCM
Rafiki yangu Rais Jakaya Kikwete atakuwa maarufu katika vitabu vya historia ya siasa kwa jinsi anavyoiongoza Tanzania kuelekea katika anguko la kiuchumi na utawala bora.
Maandishi ya kichokonozi ya Mchokonozi yatakuwa yakifurahisha vijana kuyasoma, watasoma hivi: “Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, huku akijua kuwa chama anachokiongoza kinaporomoka kutoka katika umaarufu wake kiliojengewa na walio kiasisi, alikiacha kiporomoke hadi kianguke ili chama cha upinzani chenye nguvu kiweze kushika hatamu za uongozi kwa sababu alijua kuwa hakina tena uwezo wa kuongoza.”
Wajukuu wa wajukuu wa Kikwete watakuwa wakijisifia na kulionea fahari jina la babu yao kwa sababu ya ujasili wake wa kushiriki kuua kilicho chake; CCM kwa faida ya watanzania.
Watasoma jinsi wasaidizi wake walivyojitahidi kuvuruga uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili tu kusaidia kilicho chao kiendelee kutawala, watasoma kwa mshangao mwenendo wa Bunge la Katiba na wakiwa wanajadili katika makundi yao, watakuwa wakicheka sana jinsi mchakato mzima wa uandikaji Katiba ulivyokuwa. Hapa burudani itakuwa ni Samuel Sitta.
Watoto na wajukuu zetu watasoma na kutucheka sisi sote kwa kuwa taifa la watu wa aina ya bendera fuata upepo. Watasoma historia ya serikali iliyotikiswa na Bunge hadi ikaanguka na katika maandishi hayo watamuoana rais aliyeguswa kwa mabaya na uchunguzi wa kamati ya kibunge lakini kwa sababu ya ukubwa wake, akafichiwa siri.
Historia huzungumzia mambo ya kale hivyo watakaokuwa wakizungumzwa katika historia wakati huo watakuwa hawapo. Vijana wa wakati huo hawatakuwa na woga wa kusoma na kucheka staili ya uongozi wa Rais Kikwete kwa sababu hatakuwepo. Hatakuwa rais tena.
Jengo la Bunge
Watachekeshwa na uamuzi wa bunge kuunda kamati ya bunge iliyokuwa na wabunge wenye uhasimu wa kisiasa wa baadhi ya viongozi wa serikali, ikawachunguza dhidi ya tuhuma zao kisha ikapendekeza wajichukulie hatua mwenyewe! Nao kweli wakajihukumu kwa hasira.
Historia hiyo ya kuchekesha itaonyesha jinsi baadhi ya mapendekezo ya bunge yalivyoweka pembeni na pia yalivyolisababishia taifa hasara ya mabilioni kwa sababu ya kukiuka ushauri wa kitalaamu uliotolewa na watalaamu wa fani ya sheria kuhusu namna ya kushughulikia kile kilichopewa jina la kashfa ya Richmond ambacho baadaye kilisafishwa kwa kupewa jina jipya la Dowans.  
Kwa wenye kufikiria dunia ya kesho itakuwaje, nina hakika watakuwa wanatazama na kuona jinsi watoto na wajukuu wetu wanatavyokuwa wanashangazwa na uamuzi wa wabunge kujitishwa madaraka ya ukachero, kuendesha mashitaka na uhakimu dhidi ya viongozi wa kitaifa. Kwa hakika vijana hawa watakuwa wanacheka sana.
Kila watakapokuwa wanasoma historia ya nyuma zaidi ya kupigania uhuru wa taifa letu ili tujitawale na kujiamulia mambo yetu wenyewe, hapo ndipo vijana hawa watakuwa wanavunjika mbavu kwa sababu maandishi ya miaka 50 baada ya Uhuru yatakuwa yanaonyesha kuwa bado Tanzania ilikuwa ikiamuliwa mambo yake na wazungu ambao leo wanamlazimisha rafiki yangu Rais Kikwete atekeleze maazimio kandamizi nane ya bunge dhidi ya waliohukumu hukumu ya uonevu.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya