Monday, December 23, 2024
spot_img

HISTORIA IANDIKWE UPYA SASA (1)

NI jambo la bahati mbaya sana kwamba wapo baadhi ya watu ambao husoma maandishi ya kichokonozi bila kuyaelewa na wapo pia wengine ambao husoma na kuelewa lakini husahau baada ya dakika chache.
Wiki mbili zilizopita, niliandika katika safu hii nikieleza kiunaga ubaga hatari ya binadamu kupigana vita na Simba, wengi walisoma andishi lile, lakini waliolizingatia ni wachache, na wapo pia waliosoma na kuelewa lakini baada ya dakika chache walisahau walichokisoma.
Hili linadhihirishwa na shangilio la kitoto la baadhi ya watu ambao baada ya kusikia taarifa za Mchokonozi kusimamishwa na baadaye yeye mwenyewe kuamua kujing’atua kutoka katika Kampuni ya Jukwaa la Wahariri.
Wanaoishi kwa hofu kwa sababu ya dhambi zao, waliposikia taarifa hizo walikenua meno kushangilia na waliotekeleza mpango huo walibaki wakichekea kwapani kwa furaha, wakiamini kuwa sasa wamemfunga mdomo na mikono Mchokonozi.
Wakiwa katika furaha yao hiyo, walikuwa kama vitoto vya swala vilivyokuwa vinalambalamba mkia wa  Simba dume aliyelala usingizi lakini baada ya kushtuka na kuruka kando kwa sababu ya mkia wake kuloweshwa na mate, vitoto vile vya swala vilitimua mbio kwenda kwa mama zao huku vikishangilia kwa furaha kuwa vimefanikiwa kumtisha Simba akakimbia! Utoto wa Swala.
Kwa sababu hiyo leo katika safu ya Mchokonozi nitajadili jambo muhimu ambalo limewatikisa wengi, baadhi wakibaki bila kulielewa sawasawa na wengine wakilielewa lakini wakilipotosha kwa makusudi kwa sababu ni makuwadi wa wanasiasa na wafanyabiashara wanaopigana kufa au kupona kuhakikisha kuwa ukweli wake haufahamiki. Ninajadili hili ili historia yake iandikwe upya.
Jambo hili ni habari nzito iliyoandikwa na gazeti hili katika toleo lake la Aprili 17, mwaka huu, iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Mtandao hatari,’ huku ikiwataja baadhi ya wana habari ambao duru zake za uchunguzi zilibaini pasipo shaka kuwa walikuwa wana mtandao wa aliyekuwa mtuhumiwa wa kupanga njama za ugaidi.
Lakini kabla sijafanya hivyo, nieleze kidogo kuhusu kujitoa kwangu kwenye Kampuni ya Jukwaa la Wahariri ili kuweka sahihi taarifa zinazopotoshwa na makuwadi wa wanasiasa waliojificha kwenye kivuli cha uandishi wa habari.
Binafsi, sifahamu kama kuna chombo kinachoitwa Jukwaa la Wahariri Tanzania, ninachofahamu mimi ni kwamba, kuna Kampuni ya Jukwaa la Wahariri ambayo mimi nilikuwa mshirika wake, siyo mwanachama kama inavyopotoshwa.
Mullinda (Mchokonozi)
Ieleweke kuwa, Mchokonozi hajawahi kuwa mwanachama wa Jukwaa la Wahariri, hajawahi kuwa na kadi ya Jukwaa la Wahariri, wala hajawahi kuandika barua ya kuomba uanachama au kujaza fomu yoyote ya kuomba kujiunga na Jukwaa la aina hiyo.
Ushirika wa Mchokonozi katika Kampuni ya Jukwaa la Wahariri ulikuwa sawa na ule wa kijiweni. Ajitokeze Mhariri mwenye kadi ya uanachama wa Jukwaa la Wahariri aionyeshe, akipatikana, kwanza nitaomba radhi katika safu hii kwa andishi hili ambalo nina hakika litawaumiza wachumia tumbo na kisha ninastaafu kuchokonoa.
Kampuni ya Jukwaa la Wahariri  imesajiliwa kwa wakala wa usajili wa makampuni, ina wakurugenzi wake na zipo taarifa kuwa wajanja wachache wamekuwa wakifaidika nalo kwa njia haramu.
Wanaoamini hili wanadai kuwa katika kipindi cha muda mfupi, imetumia zaidi ya sh milioni 6 kulipia vikao viwili na tiketi ya ndege na posho kwa ajili ya hao waliowaandaa kufanikisha malengo yao ya kuwashughulikia Charles Mullinda na Ratifa Baranyika.
 Wanahoji pesa hizi zinatoka mfuko gani na kwa faida ya nani? Kama ni vikao kwanini usitumike ukumbi wa MCT au ndiyo yalee mambo ya ‘ten per cent’
 Ili kulijadili kwa namna nzuri hili, linahitaji mjadala unaojitegemea. Naliweka kiporo kwa sasa.
Hata hivyo, ieleweke kuwa kuondoka kwangu katika Kampuni ya Jukwaa la Wahariri hakunipunguzii chochote bali kunanipa uhuru zaidi wa kutekeleza majukumu yangu ya kichokonozi, kunaniweka mbali na utumwa wa kutumiwa na wanasiasa na matajiri wenye malengo mabaya dhidi ya taaluma ya habari na taifa kwa ujumla.
Nirejee kwenye mjadala wangu wa leo unaohusu habari ya mtandao hatari kama ilistahili na kukidhi viwango vya kihabari. Nitaeleza kwa kirefu kidogo.
Taifa letu liko katika tishio la matukio ya kigaidi. Zipo tetesi kuwa baadhi ya Watanzania wenzetu wanajihusisha na matukio haya.
Mmoja wa waathirika wa matukio ya aina hii ni Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda ambaye kwa sasa yuko nje kwa matibabu baada ya kuvamiwa, kushambuliwa na kujeruhiwa kiasi cha kukichungulia kifo na watu ambao hawajafahamika.
Kibanda
Kwa sababu hiyo, Kibanda ni kiongozi wa waandishi na wahariri wa gazeti hili, lakini kikubwa zaidi, Kibanda ni mwalimu na kaka wa baadhi ya waandishi wa gazeti hili hili na kwa Mchokonozi, Kibanda ni kaka, mwalimu na bosi. Ni zaidi ya Kampuni ya Jukwaa la Wahariri, hivyo tatizo lililompata lilichukuliwa kwa uzito wa kipekee na wafanyakazi wote wa Kampuni ya New Habari.
Kama wanahabari wengine, waandishi wa MTANZANIA Jumatano, walichukua jukumu la kutafuta ukweli wake kwa kuchunguza mwenendo wa tukio zima, lengo likiwa kuhakikisha wahuni wanaohatarisha usalama wa watu wema wanapatikana.
Taarifa zilizokusanywa na gazeti hili kwanza zilionyesha kuwepo kwa nguvu kubwa ya baadhi ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuongozwa na wanasiasa vilivyokuwa vikiripoti mwenendo wa uchunguzi wake kwa staili ya kulishinikiza Jeshi la Polisi kutekeleza matakwa ya vyombo hivyo.
Kwa namna ya ajabu kabisa vyombo hivyo vililishambulia jeshi hilo kwa kulihusisha na tukio hilo na hapo hapo vikihusisha baadhi ya maofisa wa Serikali na wale wa Idara ya Usalama wa Taifa kuwa na mkono katika utekaji na utesaji raia.
Wakati hayo yakijiri, taarifa nyingine zilionyesha kuwepo kwa madai yaliyokuwa yakiwahusisha baadhi ya wanasiasa wenye uhusiano wa karibu na vyombo hivyo ama washirika wao na matukio ya utekaji na utesaji raia.
Ni wakati huo, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare, alipokamatwa baada ya kunaswa kwa mkanda wa video uliokuwa ukimuonyesha akipanga njama za kumteka Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msack na siku chache baadaye, kada mwingine wa chama hicho, Joseph Ludovick naye alikamatwa na kuunganishwa kwenye tuhuma zilizokuwa zikimkabili Lwakatare.
Vyombo vya habari vile vile na kwa staili ile ile vilifanya kazi yenye kutiliwa shaka kuhusu tukio hilo huku vikitoa wito wa nguvu wa kutaka waliokuwa na mawasiliano na Ludovick wahojiwe na mmoja wa hawa alikuwa mwanafamilia wa wanahabari, Majjid Mjegwa.
Ni wazi kwamba Ludovick alionekana kuwa mtu muhimu katika mpango wa kutekwa kwa Msack, kurekodiwa kwa Lwakatare na ziliibuka hisia kuwa anaweza kuwa na taarifa zenye kusaidia uchunguzi wa tukio lililomsibu Kibanda kwa sababu ilibainika alikuwa akifuatilia kwa namna ya kuchunguza nyendo za Wahariri wa aina ya Msack wanaoaminika kutonunulika na wanasiasa wanaovitumia vyombo vya habari kwa manufaa yao.
Huku shinikizo la kutaka watu waliokuwa na mawasiliano ya karibu na Ludovick wachunguzwe likiwa limeshika kasi, gazeti hili lilipata taarifa za baadhi ya wahariri waliokuwa na mawasiliano ya karibu na Ludovick, lakini hawakupata kuliweka wazi hilo kwa wanahabari wenzao na hata kwenye vikao vya Kampuni ya Jukwaa la Wahariri, hao ni Ansbert Ngurumo na Deodatus Balile.
Uchunguzi wa kina uliofanyika ulibaini kuwa Ngurumo ambaye ni mwandishi, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima na mwanasiasa anayejiwinda kugombea ubunge kupitia Chadema ni mshirika wa Ludovick kisiasa na amekuwa na mawasiliano naye ya karibu na Balile alibainika kuwa na uhusiano wenye kutiliwa shaka na mtuhumiwa huyo na kwamba ndiye aliyempatia baadhi ya taarifa za wahariri alizokuwa akizitafuta.
Ili haya yaeleweke sawasawa, twende taratibu, nianze na Ngurumo:
Ilibainika kuwa Ngurumo alikuwa na mawasiliano ya simu na Ludovick na wawili hao uswahiba wao ulifikia kiwango cha kutumiana fedha kupitia mitandao ya simu.
Kwamba Ngurumo licha ya kuwa mwandishi wa habari ni mwanasiasa aliye karibu sana na viongozi wa Chadema na pia swahiba wa aliyekuwa mtuhumiwa wa ugaidi, Lwakatare na kwa maneno yake mwenyewe Ngurumo baada ya kuulizwa na gazeti hili, alisema alikutana na kumfahamu Ludovick akiwa katika harakati zake za kisiasa na alifahamishwa kwake na Lwakatare.
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili ulibaini kuwa wakati Ludovick alidai kutekwa na kuporwa simu zake zote, Ngurumo, siku sita baada ya tukio la kutekwa na kushambuliwa kwa Kibanda aliandika katika ukurasa wake wa ‘facebook’ akieleza kuwa simu yake imeibiwa na aliyeiiba anaitumia kuibia watu fedha.
Simu yake hiyo iliyoibiwa, aliyeiiba! alikuwa akiwapigia watu na kuwaomba wamtumie fedha na anafanikiwa kuzichukua. Kwa maana nyingine mwizi huyo alikuwa na namba ya siri ya tigo pesa ya Ngurumo! Na ni simu hiyo iliyokuwa ikihofiwa kuwa alikuwa akiitumia kuwasiliana na Ludovick na hata kumtumia fedha.
Lakini pia ilibaini kuwa Ngurumo hakwenda kufunga simu yake Kampuni za simu kwa zaidi ya siku mbili isipokuwa aliripoti wizi huo kwenye mtandao wake wa ‘facebook.’
Uchunguzi katika mtandao wa simu ulibaini kuwa simu ambayo Ngurumo alidai kuibiwa yenye namba 0719 001 001, iliyokuwa bado katika safu ya bodi ya wahariri wa gazeti analoliongoza, ilikuwa imesajiliwa kwa jina la Subira Ramadhani.
Rekodi za mwenendo wa Ngurumo zilibainisha kuwa akiwa msaidizi wa Kibanda katika Kampuni ya Free Media Ltd, alikuwa akimfitini kwa watu mbalimbali kutokana na staili ya uongozi wake na ilibainika kuwa alipata kuondoka eneo lake la kazi, akasafiri nje ya Mkoa wa Dar es Salaam kwenda kuhudhuria kikao cha viongozi wa Chadema na moja ya mazungumzo yao yalimuhusu Kibanda ambaye walimtuhumu kulitumia vibaya gazeti la Tanzania Daima kwa kushindwa kuandika habari zenye mwelekeo wa kukibeba Chadema.
Kuthibitisha hilo, ilibainika kuwa Kibanda alipata kumuuliza Ngurumo kuhusu safari yake hiyo na akakubali kusafiri lakini alificha alioonana nao na walichokuwa wakikijadili.
Ilielezwa pia kuwa Kibanda amepata kuonywa na watu wanaoheshimika wapatao 10 kuhusu mwenendo wa rafiki yake ambaye ni Ngurumo kuwa hakuwa mtu mwema kwa sababu alikuwa akimsema vibaya.
Ngurumo alihojiwa na gazeti hili kupitia simu yake ya kiganjani na alikiri kuwa na uswahiba wa kisiasa na Ludovick, alikiri kumfahamu Lwakatare, alikiri kumtumia fedha Ludovick kupitia simu yake ya kiganjani na mengine yaliyoandikwa katika habari ile ya mtandao hatari.
Na katika hali ya kushangaza! Ngurumo, rafiki kipenzi wa Kibanda, kijana waliyefanya kazi pamoja kwa muda mrefu, msaidizi wake wa karibu kazini na mshirika wake katika mambo mengi hakupata kumweleza iwapo mtu anayetuhumiwa kwa ugaidi, anayehofiwa kuwa anaweza kuwa na taarifa muhimu za sakata lake ni swahiba wake wa kisiasa na kimaisha.
Ngurumo alibaki na siri hiyo moyoni mwake hata alipokwenda Afrika Kusini kumjulia hali Kibanda, aliifumbata moyoni.
Asimame Ngurumo akanushe haya. Asimame Ngurumo akimbilie mahakamani niitwe kuthibitisha maandishi yangu haya. Nipo, nataka iwe hivyo ili historia mpya iandikwe sasa.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya