Bunge la Wawakilishi la Marekani limepitisha azimio linalolenga kumzuia Rais wa Marekani, Donald Trump, kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Iran, katika ishara ya kuongezeka kwa upinzani wa kisiasa dhidi ya vita vinavyoendelea kati ya mataifa hayo mawili.
Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 215 dhidi ya 208, huku wabunge wanne wa chama cha Republican, anachotoka Trump, wakijiunga na wabunge wa Democrats kuunga mkono hatua hiyo ambayo imeelezwa kuwa imeonyesha mgawanyiko ndani ya chama tawala kuhusu mwelekeo wa vita vilivyoanza mwezi Februari.
Hata hivyo, azimio hilo bado linahitaji kupitishwa na Senate, ambalo linadhibitiwa na Republican. Endapo litapitishwa, Trump bado anaweza kutumia mamlaka yake ya kura ya turufu (veto) kuzuia azimio hilo kuwa sheria, isipokuwa mabunge yote mawili yapate theluthi mbili ya kura za kubatilisha uamuzi huo.
Wabunge wa Republican waliojiunga na Democrats ni Thomas Massie, Brian Fitzpatrick, Tom Barrett na Warren Davidson. Barrett alisema ni jukumu la Bunge pekee kutangaza vita na kwamba alipiga kura kwa kuzingatia dhamiri yake bila kujali shinikizo la kisiasa.
Kwa upande wake, mbunge wa Democrats Gregory Meeks alisema kura hiyo ni pigo kubwa kwa Trump, Akidai kuwa vita dhidi ya Iran imegharimu fedha nyingi, haijafanikisha malengo yaliyotangazwa na serikali, na imeongeza ugumu wa kufikia suluhisho la kidiplomasia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Meeks pia alisema baadhi ya wabunge wa Republican wameanza kusikiliza matakwa ya wapiga kura wao ambao hawataki kuona Marekani ikiingia katika vita vingine vya muda mrefu katika eneo la Mashariki ya Kati licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa hivi karibuni, Marekani na Iran zimeendelea kurushiana mashambulizi katika siku za karibuni.
Akizungumza kutoka Ikulu ya White House, Trump alisema mazungumzo ya kumaliza vita yanaendelea vizuri na yanaweza kufikia hitimisho mwishoni mwa wiki hii aliongeza kuwa pande zote mbili ziko karibu kufikia makubaliano yatakayomaliza mzozo huo na kurejesha utulivu katika eneo hilo.






