Mapigano kati ya Israel na Hizbullah yameendelea kushika kasi huku wajumbe kutoka Israel na Lebanon wakikutana mjini Washington, Marekani, kwa duru ya nne ya mazungumzo ya moja kwa moja yanayolenga kupunguza mvutano unaoendelea katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Lebanon, Israel imefanya mashambulizi katika maeneo takriban 30 kusini mwa Lebanon tangu Jumanne. Miongoni mwa maeneo yaliyolengwa ni mji wa Tyre, ambapo mashambulizi yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Nayo Hizbullah imesema imevishambulia vikosi vya Israel vilivyoko kusini mwa Lebanon, ikisisitiza kuwa itaendelea kujibu mashambulizi yoyote dhidi ya maeneo ya Lebanon.
Mapigano hayo yanaendelea licha ya tangazo la Rais wa Marekani, Donald Trump, aliyedai kuwa juhudi zake zimefanikisha makubaliano ya usitishaji mapigano kati ya pande hizo mbili.
Ubalozi wa Lebanon mjini Washington ulieleza kuwa makubaliano yaliyopendekezwa yangelenga awali kusitisha mashambulizi ya Israel dhidi ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut, pamoja na mashambulizi ya Hizbullah dhidi ya Israel, kabla ya kupanuliwa katika maeneo mengine.
Hata hivyo, hakuna upande uliothibitisha rasmi kukubali mpango huo. Afisa mwandamizi wa Hizbullah, Mahmud Qomati, amesema kundi hilo halitakubali usitishaji mapigano ambao haujumuishi kusitishwa kwa mapigano yote.
Mvutano huo unaendelea kuongeza wasiwasi wa kuzuka kwa mgogoro mpana zaidi katika Mashariki ya Kati, huku juhudi za kidiplomasia zikikabiliwa na changamoto ya kuwaleta pande zote mezani kwa makubaliano ya kudumu.






