Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP) umeendelea kuwajengea uwezo walimu katika matumizi ya mbinu bora za ufundishaji, hatua inayolenga kuinua ubora wa elimu ya Sayansi na Hisabati nchini.

Kupitia mafunzo hayo, walimu 281 wa masomo ya Sayansi na Hisabati kutoka mikoa ya Manyara na Kilimanjaro wamepatiwa mafunzo maalum kama sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mei 20, 2026, Afisa Elimu Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Ntumwa, amesema yanalenga kuwajengea walimu uwezo wa matumizi ya mbinu bora za ufundishaji, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na kuongeza ufanisi katika ufundishaji wa masomo hayo.

Ntumwa amesisitiza kuwa walimu wanapaswa kuzingatia maadili ya kazi, utu, uwajibikaji na kuheshimu viongozi pamoja na jamii, ili kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu bora.

Ameongeza kuwa walimu wana nafasi muhimu katika kujenga taifa lenye maarifa na maadili, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, nidhamu na uwajibikaji ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuchochea maendeleo ya elimu nchini.

Kwa upande wake, Mratibu wa mafunzo hayo, Majaliwa Mkalawa, amesema programu hiyo inawawezesha walimu kwa kuwapatia mbinu za kisasa za ufundishaji, hususan matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya kuongeza ubora wa ujifunzaji kwa wanafunzi wa shule za sekondari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here