Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amearuhusu mgogoro kati ya Kampuni ya Tarylin Limited na Travel Partner Limited uliopo Wilaya ya Karatu kupelekwa katika Mahakama ya Biashara jijini Dar es Salaam, baada ya pande hizo kushindwa kufikia muafaka wa pamoja.
Hatua hiyo imekuja baada ya pande zote mbili kushindwa kukubaliana katika kikao kilichofanyika leo Jumatatu Mei 04, 2026, katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Karatu, kilicholenga kutafuta suluhu ya mgogoro huo uliotokana na mvutano wa kimkataba kati ya mwekezaji na mpangaji.
Katika mgogoro huo, mwekezaji anadai mpangaji alikiuka masharti ya mkataba kwa kushindwa kulipa kodi ya pango, hatua iliyosababisha kuvunjwa kwa mkataba. Hata hivyo, mpangaji amepinga madai hayo akieleza kuwa hana deni na kwamba mkataba ulivunjwa kinyume na taratibu, akirejea kipengele cha 6.4 cha mkataba huo.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Makalla amesema jitihada za serikali za kuwapatanisha zimegonga mwamba kutokana na pande zote kushikilia msimamo wao.
“Pande hizi mbili zimeshindwa kuafikiana upi ukweli katika jambo hili na katika mazungumzo haya tumebaini mahusiano yameyumba. Hakuna upande wenye nia ya kufikia suluhu, hivyo tunaona njia sahihi ni kwenda mahakamani,” amesema Mhe. Makalla.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa makubaliano ya awali ya kimkataba, pande hizo zilipaswa kwanza kujaribu kutatua tofauti zao kwa mazungumzo kabla ya kuchukua hatua za kisheria, jambo ambalo halijafanikiwa huku akisisitiza kuwa hatua inayofuata ni pande hizo kwenda Mahakama ya Biashara ili kupata uamuzi wa kisheria kuhusu mgogoro huo.






