Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa unaozidi kubadilika na kuvuka mipaka huku akibainisha kuwa teknolojia ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Akizungumza leo Mei 4, 2026, wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa 11 na Kongamano la Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP) unaofanyika katika Ukumbi wa Blue Sapphire jijini Dar es Salaam, Dkt. Nchemba amesema mafanikio katika mapambano dhidi ya uhalifu uliopangwa hayawezi kupatikana bila mshikamano wa kimataifa.
Amesema katika dunia ya sasa, uhalifu mwingi hupangwa, hufadhiliwa na kuratibiwa kupitia mifumo ya kidijitali, jambo linalohitaji mifumo imara ya kiteknolojia pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya mataifa.
“Kama ambavyo uhalifu uliopangwa hauwezi kuwepo bila kuvuka mipaka, vivyo hivyo vyombo vya dola na mifumo ya haki ya jinai haviwezi kukabiliana nao kwa ufanisi bila kuwa na ushirikiano madhubuti wa kimataifa, hususan katika maeneo ya msaada wa kisheria na urejeshaji wa watuhumiwa,” amesema.
Aidha Ameongeza kuwa tafiti zinaonesha kuwa uhalifu dhidi ya wanyamapori pamoja na aina nyingine za uhalifu wa kimataifa hupangwa na kuratibiwa kidijitali, huku ukifichwa kwa mbinu tata za kiteknolojia zinazofanya shughuli hizo kuwa ngumu kugundulika kwa wakati.
Dkt. Nchemba amesema kutokana na hali hiyo, matumizi ya teknolojia ni muhimu katika kuimarisha ufanisi wa mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa, hususan katika ukanda wa Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla huku Akionya kuwa biashara haramu ya wanyamapori na aina nyingine za uhalifu wa kimataifa uliopangwa ni tishio kubwa kwa rasilimali za Taifa na unahatarisha utulivu na usalama wa nchi.






