Tuesday, December 24, 2024
spot_img

PAUL MAKENZIE: DEREVA TEKSI, MUHUBIRI ALIYETUMIA JINA LA YESU KUUA WATU ZAIDI YA 100

Makala Maalumu

PAUL Makenzie, mtu aliyejitambulisha kama muhubiri wa neno la Mungu nchini Kenya kabla ya kuangamiza maisha ya watu zaidi ya 100 kwa kuwahadaa waache kula ili wafe wakaonane ya Yesu Kristu, historia yake bado imejificha.

Tangu ilipobainika kusababisha vifo vya zaidi ya waumini wake zaidi ya 100, waandishi wa habari za uchunguzi wa vyombo vya habari vya Kenya wamefanya jitihada za kuipata historia yake kamili pasipo mafanikio.

Walichokibaini mpaka sasa ni kwamba Paul Makenzie alianza harakati za kusaka fedha katika Mji wa Malindi nchini Kenya kama dereva teksi na wengi wa waliopata kumfahamu, waliomzungumzia, wamekaririwa kuwa wakati huo akiwa dereva taksi hakudhaniwa kuwa angeweza kuja kusababisha vifo vya watu wengi katika maisha yake mbeleni.

Akijishughulisha na kazi ya udereva taksi katika Mji wa Malindi, Makenzie alioa mke wa kwanza ambaye aliachana naye na kuoa mwingine wa pili ambaye pia walichana kabla ya kuoa mke wa tatu ambaye ndiye aliyehama naye kutoka Malindi kwenda kwenye shamba lake huko Shakahola.

Inaelezwa kuwa mwanzoni mwa miaka 2000 aliachana na kazi yake ya udereva teksi na kuanzisha kanisa aliloliita Good News International Church ambalo mpaka mwaka 2003, lilianza kuwavutia watu wengi na hapo alianza kubadilisha mafundisho yake kutoka kwenye kitabu cha biblia ya kikristu na kuanza kuwafundisha waumuni wake ujunga.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa kutoka vyombo vya habari mbalimbali vya nchini Kenya, mwaka 2003 Makenzie alianza kuwafundisha waumini wake kuichukia elimu na waliosoma aliwataka wachome vyeti vyao vya elimu.

Makenzie aliwafundisha waumini wake kuchukia dini nyingine na hapo alipoteza baadhi ya waumini ambao waliamua kuachana naye lakini wapo wengine wengi waliobakia naye kama wafuasi wake, wakiamini kile alichokuwa akiwafundisha.

Taarifa nyingine zinaeleza kuwa baadhi ya raia wa Kenya waliwatoroka ndugu na jamaa zao kwenda kujiunga na Kanisa la Makenzie kwa siri lakini hadi sasa haijajulikana ni kipi hasa kilichowavutia kwa Makenzie hadi kufikia uamuzi wa kutoroka familia zao na kwenda kwake.

Akiwa tayari na waumini wengi, Makenzie aliwafundisha waumini wake kutowapeleka watoto shule na hata walipougua aliwakataza kuwapeleka hospitali kupatiwa matibabu.

Makenzie aliendelea kuimarisha kanisa lake kwa kukusanya wakenya wengi hadi mwaka 2019 alipoingia kwenye mgogoro na Serikali ya Kenya kutokana na mafundisho yake na baada ya kubanwa alilifunga kanisa lake lakini hakuwaacha mkono wafuasi wake, bali aliendelea na shughuli zake za kuhubiri mafundisho potofu kwao kwa njia ya siri.

Katika harakati zake hizo alipata kukamatwa mara kadhaa na hadi anakamatwa kwa kosa la kusababisha vifo vya raia wengi wa Kenya kwa kuwataka wasile chakula ile wafe wakaonane na Yesu, alikuwa akikabiliwa na kesi nyingi mahakamani.

Makenzie baada ya kufunga kanisa lake katika Mji wa Malindi alikuwa akieleza kuwa sababu ya kulifunga ni kukamilisha kazi yake ya unabii wa nyakati za mwisho kama alivyoagizwa na Mungu.

Baadaye uvumi uliokuwa miongoni mwa wakenya kuwa Makenzie alikuwa amehamishia kanisa lake eneo la Shakahola ambako alinunua ardhi yenye ukubwa wa ekari       800 ambayo waumini na wafuasi wake walikuwa wakilima huku wakisubiri kurejea kwa Yesu Kristu kulithibika kuwa ni kweli baada ya kugundulika kwa miili ya watu waliokuwa wamekufa kwa njaa baada ya kuambiwa na Makenzie wasile ili wafe wakakutane na Yesu Kristu.

Makenzie ambaye alifunga kanisa lake katika Mji wa Malindi, alilihamishia kwenye shamba kubwa lenye ukubwa wa ekari 800 na huko aliishi na wafuasi wake waliokuwa wakimtumikia kwa kulima shamba na pia alichukua mali zao kwa kuwahadaa kuamini kuwa dunia iko kwenye nyakati za mwisho, hivyo wajiandae kuonana na Yesu Kristu.

Kwa mara ya kwanza, makaburi 14 waliyozikwa watu wengi waligundulika kwenye shamba la Makenzie wiki iliyopita. Shirika la Utangazaji wa Uingereza (BBC) linamkariri mwanaharakati wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu linalofahamika kwa jina la Haki Afrika, Hussein Khalid akieleza kuwa ameshuhudia miili mingi ya watu ikifukuliwa kwenye makaburi waliyozikwa pamoja.

Khalid anakaririwa kuwa eneo lenye makaburi hayo ni ndani kabisa ya shamba la Makenzie, mahali penye uficho na marehemu walikufa kwa njaa baada ya kuaminishwa na Makenzie kuwa wafunge kula chakula kama maandalizi ya kufa kisha kwenda mbinguni kabla ya kufika kwa mwisho wa dunia.

Khalid ambaye amekuwa sambamba na wafukua makaburi ndani ya msitu ulio kwenye shamba la Makenzie huko Shokahola anakaririwa zaidi kuwa katika eneo hilo anakadiria kuwepo kwa maeneo yapatayo 60 yenye makaburi ya halaiki na kwamba eneo hilo ni moja ya tano ya eneo la shamba la Makenzie lililochunguzwa.

Taarifa za awali za polisi zinaeleza kuwa watu 29 wamepatikana wakiwa hai lakini kati ya hao, siyo wote waliotaka kuokolewa na kifo kwa sababu ya imani waliyojengewa na Makenzie ndani ya mioyo yao kuwa dunia inafikia mwisho, hivyo wafe mapema ili waende mbinguni.

BBC inamkariri Khalid kuwa, jumapili iliyopita akiwa eneo hilo alikutana na mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 20 aliyeonekana kudhoofika kwa njaa lakini hakutaka msaada wake na badala yake alitaka amuache afe ili aende mbinguni.

“Tulijaribu kumpa huduma ya kwanza kwa kumnywesha maji yenye glukosi kwa kijiko lakini alikataa kabisa. Alifunga mdomo wake na alikuwa akiashiria kwa alama kuwa hataki msaada wa aina yoyote,” anakaririwa Khalid.

Anaendelea kuwa “tulikutana pia na mwanamume mmoja mwenye umri wa kama miaka 40 hivi ambaye licha ya kuwa dhaifu lakini alikuwa anaongea, yeye alisema hana akiba yoyote na kwamba alikuwa timamu na anajua anachokifanya hivyo aachwe peke yake na alidiriki kutuita maadui zake wa kwenda mbinguni.

Victor Kundo wa Kituo cha Haki za Binadamu cha Malindi ambaye anashiriki kazi ya kufukua miili katika shamba la Makenzie, yeye amekaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa anakadiria kuwepo kwa miili ipatayo 150 katika eneo hilo.

Akizungumzia jinsi taarifa za kuwepo maafa hayo alivyozipata, Kundo anasema shirika lake lilipigiwa simu na mtu aliyetaka msaada wa kuwaokoa watoto wake watatu waliokuwa chini ya himaya ya Makenzie na maafisa wa shirika hilo walikwenda eneo hilo lakini walifanikiwa kumuokoa mtoto mmoja tu.

“Ilikuwa bahati mbaya sana kwa sababu tulimuokoa mtoto mmoja tu ambaye tulimkuta ndani ya nyumba akiwa amefungwa kamba. Mtoto huyo ana umri wa kama miaka sita lakini dada yake na kaka yake tulikuta wamekwishakufa na kuzikwa jana yake.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya