RIPOTA PANORAMA
WANASHERIA wameshauri tuhuma zinazomuandamana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithinaasheri Jamaat (KSIJ) iliyopo Mkoa wa Tanga zichunguzwe na wakati huo huo ashtakiwe kwa makosa yenye ushahidi na mashahidi waliopo.
Ushauri huo wameutoa kwa nyakati tofauti wakati wa mahojiano yao na Tanzania PANORAMA Blog yaliyofanyika jana na juzi kuhusu tuhuma anazoelekezewa Walje, kauli ya Msajili wa Jumuiya wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Kihampa kuwa migogoro ya kidini inayofikishwa serikalini hushughulikiwa kwa siri na jinsi polisi walivyoingilia kati suala hilo wakiwa na mwelekeo wa kuzuia lisiripotiwe.
Walje anatuhumiwa kuwatumia washirika wake wakiwamo watoto, ambao hawajatimiza umri wa miaka 18 kuchota mamilioni ya fedha za KSIJ Tanga kutoka Benki moja ya Jijini Tanga kinyume cha taratibu, kudhulumu fedha za watu masikini wanaosaidiwa na KSIJ Tanga. Katika hili, Walje anadaiwa kuwapatia kiasi kidogo cha fedha masikini hao kisha kuwalazimisha kusaini vocha zilizoandikwa kiasi kikubwa cha fedha.
Aidha, Walje anadaiwa kupoka uongozi wa KSIJ Tanga kwani hakuchaguliwa na wanajumuiya kuwa mwenyekiti wao na kwamba baadhi ya washirika wake ambao pia wamekuwa wakimkingia kifua asiondolewe kwenye uongozi, rekodi zao ni mbaya.
“Yapo mambo ambayo yanashangaza sana. Hilo jambo tumelisoma sana maana jambo likishaingia kwenye vyombo vya habari na hasa mtandaoni linasambaa kwa kasi. Kwangu mimi kwa sababu nipo huko siyo sahihi kupingana na Msajili wa Jumuiya lakini ukijiuliza huu usiri aliousema ni wa nini? maana sote tunaona jinsi dini zinavyotumiwa sasa na watu wasio wema kujinufaisha na hata kuanganiza watu.
“Huyu mtu anatuhumiwa kunyang’anya watu stahiki zao, watu masikini tena kwa maandishi. Ile vocha tumeiona ikiwa na viwango viwili tofauti vya fedha. Huyu mtu kwanini anawafanyia hivi watu masikini? Kweli ni kiongozi wa jumuiya au amekwenda hapo kuiba na kudhulumu watu? Hivi huyu mtu mpaka sasa baada ya hayo yote kuwekwa hadharani anapaswa kuwa bado kiongozi au anapaswa kuwa amefikishwa mahakamani kujibu hicho alichokifanya?
“Lakini ni huyu huyu anayedaiwa kuchota mamilioni ya fedha za jumuiya benki na haijulikana anayatumia kwa njia zipi tena anadaiwa kutumia mpaka watoto wadogo kuchota fedha hizo. Ni kwanini vyombo vya dola havichunguzi mambo mazito kama haya?
“Maswali ni mengi lakini jambo la kwanza linalokuja akilini haraka haraka ni kwamba huyo yupo hapo kwa ajili ya kuchota hizo fedha za jumuiya lakini anachukua na za masikini na haina shaka yupo pale na wenzake ambao wana madhumuni yao. Ila mimi usiweke jina langu maana sitaki ionekane tunapingana.
“Ikitokea kama ulivyoandika, na inashangaza sana polisi kuwabana waandishi wa habari wanaoibua mambo kama haya badala ya wao kuyatumia kuzuia uhalifu, wanageuka wanashiriki kuwakandamiza wanaowasaidia.
“Na imesemwa na kiongozi muhusika kuwa mambo hayo ni ya siri, acha yawe siri lakini hakuna siri ya kudumu kwa mambo ya jumuiya, yatakuwa wazi tu na hata kama analindwa sasa utafika muda atafikishwa mahakamani tu kwa sababu alipaswa kuwa amekwishashitakiwa huyu kwa namna habari zake zinavyoelezwa,” alisema mwanasheria aliyeomba jina lake kuhifadhiwa.
Wakili wa kijitegemea ambaye alizungumza kwa sharti ya jina lake kuhifadhiwa alisema; “Mabadiliko yanakuja, ngoja tume ya haki jinai imalize kazi yake naamini hizi kadhia mnazokutana nazo waandishi wa habari zitabaki historia.
“Mimi kama mwanasheria jambo la kwanza naangalia historia ya mtuhumiwa, hapo naona ana historia ya kutenda kosa la jinai, kosa la wizi friza na alishtakiwa mahakami kwa kosa la wizi, akatiwa hatiani na mahakama, ikamuhukumu. Ndipo narejea kwenye nyaraka zilizowekwa wazi za yeye kudhulumu mali za masikini tena kwa maandishi, mtu kama huyu hata kama sizungumzi kama mwanasheria, mamlaka husika ambazo zilikwishafikishiwa malalamiko yake zilipaswa kuwa zimekwishachukua hatua.
“Na polisi kama walifanya uchunguzi, wakabaini hicho walichobaini wanasita nini kusema walichokibaini? Tuhuma za kwenda benki kuchukua fedha tena kwa kuwatumia watoto wadogo siyo za kufumbia macho. NGO ambayo haiwasilishi hesabu zake kwa Serikali kila robo mwaka kama sheria inavyotaka na viongozi wa mkoa wapo kimya. Inashangaza.
“Halafu mnaandika Walje anatuma picha akiwa na viongozi wakuu, hivi polisi hawashtuki wakamchunguza huyu mtu? Mpaka leo yupo tu hafikishwa mahakamani wakati hilo tu la kuibia masikini anapaswa kulijibu mahakamani? Polisi hawajiulizi huyu mtu ana maana gani? Ni mtu wa aina gani? Badala ya kumwita yeye kumuhoji na nyie mkawa mashahidi wanageuzia kibao waandishi. Lakini kama nilivyosema tumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda tume ya haki jinai, ikikamilisha kazi yake haya yote yataisha,” alisema.
Tanzania PANORAMA Blog amejikuta katika wakati mgumu wa kuitwa na kuhojiwa na polisi huku ikitakiwa kukabidhi ushahidi ilionao kuhusiana na sakata la tuhuma zinazomuandamana Walje na aidha, wanasheria wake wamekuwa wakitishia kuishtaki mahakamani kwa kuanika madudu yake.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga hadi sasa halisema uchunguzi wa tuhuma hizo umefikia wapi na badala yake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi (ACP) Henry Mwaibambe alieleza kutofahamu lolote huku akiahidi kufuatilia na kutoa kauli lakini baada ya hapo hajapatikana kuzungumzia hilo.
Tanzania PANORAMA Blog inazo taarifa zinazodai kuwa RPC Mwaibambe alikwishakabidhiwa faili la mgogoro wa KSIJ Tanga naye baada ya kulipitia alimuita Walje ofisini kwake kwa mahojiano na baadaye aliwaita baadhi ya waandishi wa Mkoa wa Tanga (Tanzania PANORAMA haikuitwa) na kuzungumza nao kuhusu suala hilo.
Aidha, inadaiwa Septemba 12, 2022 Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Emmanuel Kihampa aliuandikia barua uongozi wa KSIJ Tanga akiutaka kufika ofisini kwake kuzungumzia malalamiko ya wazee, wajane na watu wenye ulemavu wanaosaidiwa na taasisi hiyo lakini agizo lake hilo lilitupwa kapuni na Walje anayedaiwa kuiongoza jumuiya hiyo peke yake kama mwenyekiti.
Kihampa alipozungumza na Tanzania PANORAMA kuhusiana na hilo alisema mambo ya jumuiya za kidini hawezi kuyazungumzia kwenye vyombo vya habari kwa sababu ya kulinda hadhi na heshima za jumuiya za aina hiyo.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Tanga, Omary Mgumba wakati akizungumzia sakata hilo, pamoja na mambo mengine alisema atauita uongozi wa jumuiya hiyo ofisini kwake kuzungumzia tuhuma dhidi ya Mwenyekiti Walje za kufuja fedha za umma zilizochangwa kusaidia makundi ya wazee, wajane na wasiojiweza.
“La kwanza kwa sababu kuna tuhuma hapo za kufujwa kwa fedha za umma zilizochangwa kusaidia makundi hayo, sisi kama Serikali nafikiri hiyo ni NGO’s, shirika lisilokuwa la kiserikali na kwa kuwa ndiyo unanipa taarifa, nilikuwa sina taarifa kuhusu hilo suala, naomba nilifanyie kazi.
“Sisi kama Serikali na kwa sababu kuna jinai na wana utaratibu wa kuleta taarifa zao na hizo bado ni tuhuma hazijathibitishwa, basi ngoja tupate taarifa ya kwao hiyo taasisi kwa mujibu wa sheria kwa sababu wanatakiwa walete taarifa kila robo mwaka na Katibu Tawala wa Mkoa ndiyo mratibu wa mambo hayo basi nitaomba taarifa hiyo waniletee,” alisema Mgumba.