NI MIKITO YA KASWIDA NA MAPAMBIO

0
206
Simba Gembagu Ngw’ana Njamiti
MIKITO ni kukita na kukita ni kukitwa. Huo ndiyo mwenendo wetu watanzania wa zama hizi za bora liende.

Kila mahali ni mikito, watanzania wanakita na kukitwa. Wanakitana wanasiasa kwa staili ya upekepeke wakigombea ulaji. Wanakitana wanataaluma kila mmoja akitaka kuonyesha usomi wake hata kama ni kihiyo na watu wa Mungu nao wanakitana kwa staili mpya ya nikikita ninakitwa na nikiikita, ninaikita.

Kwa staili hii ya kita nikukite, wanafanya dhambi ya kukitana ambayo mtikisiko wake husababisha maangamizi kwa jamii nzima; na kwa sababu ya uzito wa mitikisiko ya mikito hutikisa huku na kule pasipo kikomo, wanaotikisika hukosa fursa ya kujikita sawia ili wasitikiswe na mikito hadi wanapokuwa wamekitwa na kuangamia.

Huangamia kwa kujikita katika imani ambayo ikikitwa, inatikisika.

Watu wa Mungu waliojikita kwenye imani mbili tofauti sasa wanakitana. Waliojikita katika imani ya kaswida wamekita wakakita na waliojikita katika imani ya mapambio nao wamekita wakakita.

Wote hawa wanakitana kiimani, wanakitana kutetea imani wasizojua chimbuko lake. Walizaliwa wakasadikishwa kuamini pasipo kuona. Ni vipofu waliopofuliwa na imani ya kusadikika, walisadikishwa kuamini kuwa imani yao ni mbaya wakaamini wakasadikishwa kuamini uzuri wa imani za kigeni.

Imani ni upofu na kwa sababu walipokea imani za kigeni walipofuka. Kwa vile ni wanaangamizana bila kuonana.

Hawa ni wale wanaoamini katika kaswida na mapambio, wanadhani umahiri wao wa kuimba kwa sauti kubwa kaswida na mapambio ndiyo liwazo tosha la mioyo yao linaloweza kulegeza ukakasi wa dhambi ya kuendekeza udini waliorithishwa mababu wa babu zao na wageni waliokuja kuwatia upofu ili wasiione nchi ya ahadi.

Nchi waliyomoyo, yenye mito inayotiririsha maziwa na asali lakini kwa sababu ya upofu wao wanainajisi kwa dhambi ya kukumbatia udini ambayo adhabu yake ni mauti.

Dhambi ni dhambi, hakuna dhambi kubwa wala ndogo. Kuzini na kuiba zote ni dhambi, kuchinja au kuponda kichwa kwa nyundo yote ni matendo ya kuua ambayo bwana mkubwa hayapendi.

Hilo wanalijua wauao kwa kuchija au wale wa kuponda na nyundo. Kwa Mungu hakuna chukizo lenye nafuu, kwake yeye siku zote mshahara wa dhambi ni mauti.

Wapumbavu wanaokita na kukitwa wamejikitika kutenda dhambi ya kujikunyata katika mbawa za udini wakiamini kuwa dhambi hiyo hukumu yake ina ahueni mbele ya bwana mkubwa. Wanatenda kosa la kiimani na hukumu yao imeanza kutolewa hapa hapa duniani.

Kwa sababu ya upumbavu wao wa kujikita katika imani pasipo kuikita, badala ya kuchinja wanyama sasa wanachinjana wao kwa wao. Watu wanaoihubiri imani wasiokuwa na imani. Wadhambi waliojivika joho la utume wa kuipigania imani wasiyoijua, imani iliyoletwa na wageni. Imani ya kuiga sasa inawaangamiza.

Hakuna mtanzania ambaye asili ya babu wa mababu zake ilijikita katika imani ya kaswida au mapambio. Sote tu wajukuu wa wapagani ambao imani yao haikujikita katika kujichija au kuchijiwa.

Hakuwepo babu wa mababu zetu au bibi wa mabibi zetu aliyeamini katika hukumu ya kutwangana mawe hadi kifo na kamwe hakupata kutokea aliyeamini katika kuua kwa sababu ya kutetea imani yake.

Mungu hakuutumba ili tuuane, bali tuzaane na kuongezeka ili tuujaze ulimwengu lakini sisi tumeasi agizo lake kwa kuiga utamaduni wa kigeni wa kuamini kaswida na mapambio. Mafundisho ya wageni waliyotuletea ili kutupofua tujiangimize bila kuona.

Tukubali au tusikubali, ukweli ni kwamba tumetenda dhambi ya udini ambayo msingi wake ni ubaguzi. Tumejibagua kidini, hawa wanakaswida wale wanamapambio. Babu yetu mchonga meno alipata kunena enzi za uhai wake kuwa dhambi ya ubaguzi ukiishaitenda huwezi kuiacha, ni lazima utaendelea kuitenda.

Dhambi hiyo sisi tumeitenda, tumejibagua kwa dini zetu, hawa wanakaswida na wale wanapambio na waasisi wa dhambi hii ndiyo wanaotutawala. Waliiasisi huku wakijua kuwa itatumaliza lakini kwa sababu ya tamaa yao ya madaraka, waliiumba ikajiumba, tukaipokea, ikakaa kwetu, imetuzoea na sasa inakaa nasi.

Wakiwa waathirika wa urithi wa mapokeo ya imani za kigeni zilizojikita ndani ya mioyo yao, walipoutamani ubwana kuliko utwana walihubiri udini ili wawe mabwana. Waliutafuta ubwana kwa ncha ya upanga, wakahubiri upendeleo kwa wanakaswida wakidhani wanamapambio hawapendi kupendelewa. Walifanya hivyo wakijua kuwa kuhubiri upendeleo ni dhambi kwa sababu upendeleo mwandani wake ubaguzi.

Wakiwa madarakani, ubaguzi umeota mizizi kwa msaada wa ahadi ya upendeleo walioyoitoa. Hawawezi kuuzuia kwa sababu waliukaribisha, sasa wanajaribu kuupunga hewani lakini haupungiki.

Dhambi ya ubaguzi huangamiza wote. Watawala wakiwa wametambua hilo wamesitisha utekelezaji wa maboresho ya uimbaji kaswida waliyoahidi kwa shinikizo la wanamapambio. Huo ndiyo mwanzo wa chuki baina ya watawala na wanakaswida.

Chuki inayojengwa katika msingi kuwa sitisho hilo ni shinikizo la wanamapambio imeota mizizi. Wanandugu wanaobaguana kwa imani za kidini wanawindana kwa majambia kwa kadiri ya mafundisho ya dini za kigeni. Sasa wanaangamizana kutokea visiwani.

Dhambi ya ubaguzi haiishi. Waliokitana kwa sababu ya kulilia uhalali wa kutambulika kisheria kaswida na mapambio sasa wanakitana wakigombea kuchinja. Utoto uliopitiliza.

Kwa sababu ya kuendekeza imani za kigeni, wanaoamini katika kaswida wanashinikiza watambuliwe kuwa wao tu, wapo peke yao, ndiyo wenye uhalali wa kuchinja kwa sababu tendo hilo limehalalishwa katika imani waliyorithishwa na wageni.

Hawazungumzia asili yao kama inawahalalisha wao peke yao kuwa ndiyo wachinjaji, wanazungumza imani ya mapokeo kuwa ndiyo inayowahalalisha kuwa wachijaji.

Kwa staili ile ile ya wanakaswida, kundi la wanamapambio linalokitwa lisichinje limejikita kulilia uhuru wa ruhusa ya kuchinja, halitaki kichijiwa, kisa imani ambayo msingi wake ni ubaguzi.

Linajielekeza katika dhambi ile ile ya ubaguzi ya kuweka maneno ya imani ya dini ya kigeni katika maeneo yao ya kuchinja. Kwa kuendekeza mapokeo ya imani za kigeni zilizojikita katika ubaguzi linatenda dhambi ya ubaguzi.

Watawala walioutafuta utawala kwa mahubiri ya ukabili ambayo mtoto wake ni udini wameshindwa kuwaepusha watawaliwa na adhabu ya mauti kwa kosa la kutenda dhambi ya ukabila. Wanayo misahafu iliyoandikwa na mababu zetu  ikieleza misingi ya kufuatwa katika kuuishi utanzania lakini wameshindwa kuitumia.

Wote wanajua kusoma na kuandika. Wanasoma ndani ya mistari ya misahafu hiyo na hawaoni mahali palipoandikwa ni kundi lipi kati ya haya yaliyojikita kuamini imani za kigeni linalopaswa kujicha na linalopaswa kuchijiwa. Wamebaki kuwayawaya kwa sababu ni washirika wakuu wa dhambi ya ubaguzi.

Wakati watawala wakiwayawaya kwa kuasisi dhambi ya udini na ubaguzi, wanaobaguana, wanakaswida na wanamapambio wanaoendelea kukitana. Wakitapo wanakaswida wanakitwa na wanamapambio.

Kwa sababu tumeanza, mwendo utakuwa huo wa mikito ya kukita na kukitwa hadi ukamilifu wa dahali. Ni kama vile ilivyokuwa kwa wenzetu waliojita mapema kabla yetu kwa dhambi hii hii ya udini na ubaguzi.

Majuto ni mjukuu, kwa pamoja tunapaswa kujutia dhambi ya ubaguzi tuliyoitenda wakati tukiendelea kuadhibiwa kwa dhambi hiyo ili siku ya hukumu, tuhurumiwe kwa kukikatana wenyewe kwa wenyewe. Wanaodhani adhabu yetu haijafika basi hao hawajakitwa, wakikitwa nao watajikita kuamini jambo hili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here