Monday, December 23, 2024
spot_img

Ndani Giza Nje Mimba

SIMBA GEMBAGU NG’WANA NJAMITI

KILA nikikita ninakitwa. Popote ninapokita napokewa na mikito. Napokewa na mikito halisi ya kitanzania inayonikita.

Ninakita ili nijikite lakini sijikiti badala yake ninakitwa. Ninatafuta pa kukita ili nipate pa kujikita na kuutangazia ulimwengu kuwa ingawa nimekuwa nikiweweseka kwa muda mrefu kutokana na kukosa mahali pa kukita, sasa nimepapata. Nimejikita.

Baada ya kukita huku na kule pasipo kujikita, majuzi nilikita kwenye takwimu za matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana ili nione kama kuna uwezekano wa matokeo ya sensa hiyo kutoa mwanga wa kuboresha maisha ya watu na hivyo kunipa fursa ya kujikita kutumia matokeo hayo kuhubiri matarajio ya kupatikana neema kwa Watanzania.

Lakini matokeo ya takwimu ya sensa yalinimaliza nguvu. Nikiwa nimejikita kuyaperuzi, nilijikuta ninakitwa na ongezeko kubwa la mimba za utotoni na ukubwani.

Kwangu mimi jambo la maana nililoliona kwenye matokeo yale ni ongezeko kubwa la watu ambalo chanzo chake ni Watanzania wenyewe kupeana mimba bila mpangilio.

Na nilipojikita kuchunguza chanzo cha Watanzania kujazana mimba kama hawana akili nzuri nilibaini kuwa ni mikito ya ukakasi wa maisha inayozidi kukita kila kukicha.

Hebu twende pamoja ili kila ninapokita tukite pamoja. Tuzikite akili zetu kufikiri pamoja kwa kawaida tu kuwa ni kwanini Watanzania wanapeana mimba kwa fujo kiasi cha takwimu za hesabu yao kuonyesha kuwa wameongezeka kwa kasi wakati kasi ya ukuaji wa uchumi wao na ustawi wao kisiasa vikididimia.

Tuzifikirishe akili zetu kuwa ni kwanini Watanzania wanazaliana sana licha ya kutokuwa na uhakika wa maisha yao ya kesho! Majibu ya haraka ingawa ni mepesi yanayopatikana ni haya.

Mosi; ukosefu wa kazi. Kwamba Watanzania wengi bila kujali kama wanapenda kufanya kazi au lah! Mara nyingi wanakuwa hawana kazi za kufanya kwa sababu ama hawataki kufanya kazi au wakati mwingine wanakuwa hawana kazi ya kufanya.

Watanzania hawataki kufanya kazi kwa sababu wamekulia katika mazingira ya kutofanya kazi. Siyo wote lakini wengi wamekulia katika mazingira ya aina hiyo. Kwao hawa, maisha yanakwenda kiujanja ujanja.

Wanaingiza fedha kwa kupiga porojo. Haijalisha kama porojo hizo zinaweza kutafasiliwa kuwa ni utapeli au lah! Muhimu ni kwamba hiyo ndiyo staili yao ya maisha.

Watanzania hawa wavivu wa kufanya kazi wana bidii ya kupeana mimba. Mazingira wanakopigia porojo yanahamasisha upeanaji mimba kwa sababu mara nyingi wanakuwa baa au sehemu nyingine za starehe. Inaeleweka, starehe ni pamoja na kugawiana mimba.

Pili; giza. Haina shaka hata kidogo kuwa mimba nyingi zinatungwa gizani, haijalishi kama ni mchana au usiku lakini ni kawaida kwa watu wengi wanapotaka kugawiana mimba kujifungia sehemu yenye giza.

Hata kama ni mchana kukiwa na mwangaza mkali wa jua shurti milango na madirisha vifungwe ili kuwe na giza. Kama ni mwanga basi utaruhusiwa kuwepo kidogo sana.

Sasa Tanzania nishati ya umeme imekuwa ikipatikana kwa kudra za Mwenyezi Mungu. Sijui Serikali inaichukuliaje hali hii ya ugiza.

Kuna mamia ya Watanzania wanaopenda kufanya kazi lakini wanashindwa kwa sababu ya kukosa mwanga unaozalishwa na nishati ya umeme ambayo Serikali imeshindwa kuhakikisha upatikanaji wake wa uhakika.

Ni kama vile wakubwa wanapenda Watanzania wagawiane mimba kwa wingi ingawa hawataki kusema hivyo wazi. Wanachokifanya kuhakikisha hilo linawezekana ni kutoa kauli zilizopinda pinda kuhusu hali ya giza iliyopo.

Mfano wa kauli zilizopinda ni ile iliyotolewa na profesa anayesimamia upatikanaji wa umeme ambaye alitangaza hivi karibuni kuwa kwa sababu yeye ni profesa na amechaguliwa kusimamia umeme ambao kwa miaka nenda rudi umekuwa adimu kupatikana, atauprofesa umeme ili upatikane kwa uhakika. Hautakosekana tena.

Ajabu! Umeme umeuprofesa uprofesa wake, umeendelea kutopatikana. Kukatika kwa umeme bila mpangilio kunakoendelea sasa sehemu mbalimbali nchini kunadhihirisha hili. Kwamba kauli ya profesa ilikuwa imepinda.

Hivyo kwa sababu ya giza, watu wakiwa majumbani hawawezi kuangalia televisheni au kusikiliza redio na badala yake hujifungia vyumbani mapema na kulala gizani. Matokeo yake ndiyo hayo, mimba.

Sasa; kwa sababu Watanzania wengi hawana kazi za kufanya kwa sababu ya wavuvi au sababu nyingine yoyote na kwa sababu wakubwa wameshindwa kuwawezesha Watanzania wengi kufanya kazi na badala yake wanashinda wakisogoa sehemu zao za kazi.

Na kwa sababu watu wengi wanapenda simulizi za kupeana mimba, nani kafumaniwa na nani kachumbiwa na nani, kaolewa au yuko na nani. Matokeo ya maongezi haya huwasukuma kujikita katika kugawiana mimba.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya