Tuesday, December 24, 2024
spot_img

MAJALIWA AHIMIZA MSHIKAMANO KUIJENGA CCM

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa


*Ataja miradi ya maendeleo iliyotekelezwa awamu ya sita

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

MJUMBE wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wana-Ruangwa waendelee kushikamana ili kukijenga Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kukifanya kibaki kuwa na nguvu.

Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa ametoa wito huo leo wakati akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wilayani Ruangwa kutoka kata 22 uliofanyika kuwachagua viongozi wa wilaya hiyo.

“Nasisitiza haya kwa sababu hata Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wa Taifa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametaka wanachama tushikamane, tujenge upendo miongoni mwetu na tusimamie chama chetu ili kiwe na nguvu katika maeneo yetu.

“Kama eneo la Ruangwa litakuwa na nguvu, Nachingwea litakuwa na nguvu, Liwale litakuwa na nguvu, Kilwa litakuwa na nguvu, Lindi Vijijini na Manispaa yatakuwa na nguvu, Mkoa wa Lindi automatically utakuwa na nguvu kisiasa na mimi naamini Ruangwa hatutamwangusha Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo mafanikio yaliyopatikana wilayani humo chini ya Serikali ya awamu ya sita ikiwemo ujenzi wa shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, miradi ya maji, chuo cha VETA, mabweni ya wanafunzi wa sekondari, maji na umeme.

“Sisi Wilaya ya Ruangwa tumetekeleza vizuri Ilani ya CCM na Rais Samia ametuunga mkono sana. Nani hajui kama wilaya hii ilikuwa na upungufu mkubwa kwenye sekta ya elimu? Nani hajui kwamba hatukuwa na shule za msingi katika kila kijiji? Lakini leo tumejitahidi na tumefikia zaidi ya asilimia 90. Ahadi ni kuhakikisha mpaka kufikia mwaka 2025, kila kijiji kinakuwa na shule ya msingi,” amesisitiza.

Akifafanua zaidi kuhusu elimu, Majaliwa amesema kulikuwa na kata tatu za Mbwemkuru, Nandagala na Nanganga ambazo zilikuwa hazina shule za sekondari lakini hivi sasa kila kata imepewa Sh. milioni 470 na ujenzi umeshaanza.

“Pia tumepewa shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa shule maalumu ya wasichana watakaochukua masomo ya sayansi. Shule hii iko Ruangwa, nyuma ya uwanja wa mpira wa Majaliwa na itaanza kufundisha kuanzia Januari, 2023,” asema.

Amezitaja shule nyingine zilizojengwa kuwa ni ya Kitandi ambayo pia itaanza kufundisha kuanzia Januari, 2023. “Wilaya hii, watoto wetu wa kike bado wana changamoto nyingi kwa vile Liugulu kuna sekondari mbili, tumeamua moja iwe na wavulana na nyingine iwe ya wasichana na zote hizi tunazijengea mabweni ili vijana wetu wapate malezi mazuri shuleni,” amesema.

Amesema wilaya hiyo ilipokea Sh. bilioni mbili za ujenzi wa Chuo cha VETA na kuwaarifu wajumbe hao kwamba wamepata eneo la ekari 70 na ujenzi wake umekamilika isipokuwa wanasubiri kuingiza maji.

Kuhusu afya, Majaliwa amewaeleza wajumbe hao kuwa ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo imefikia hatua nzuri na vituo vya afya vya Luchelegwa, Nandagala, Ruangwa, Narung’ombe, Nangurugai, Namichiga na Mandawa umekamilika. “Itabakia kata moja ya Nambilanje,” amesema.

Kuhusu umeme, Majaliwa amesema kazi ya kusambaza umeme vijijini inaendelea na lengo la wilaya ni kuhakikisha ifikapo Disemba 2022, vijiji vyote viwe vimepata umeme.

Uchaguzi huo unahusisha nafasi ya Mweyekiti wa CCM wa wilaya, wajumbe watatu wa Mkutano Mkuu Taifa, wajumbe 10 wa halmashauri kuu ya wilaya na wajumbe wawili wa halmashauri kuu ya mkoa.

 

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya