Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza katika maeneo mbalim bali nchini Afrika Kusini wakitaka serikali ichukue hatua kali dhidi ya wahamiaji wanaoishi nchini humo bila vibali halali.
Maandamano hayo, yanayotajwa kuwa makubwa zaidi tangu wimbi la mashambulizi dhidi ya wahamiaji mwaka 2008, yalifanyika kwa amani kwa kiasi kikubwa licha ya kuripotiwa matukio machache ya uporaji ambapo Polisi waliwakamata watu kadhaa kuhusiana na matukio hayo, ingawa idadi kamili ya waliokamatwa haijawekwa bayana.
Kwaupande wake Waziri wa Sheria nchini humo, Mmamoloko Kubayi, amepongeza utulivu uliotawala wakati wa maandamano hayo, huku akionya kuwa mtu yeyote atakayehusika na vurugu au vitendo vya uhalifu atachukuliwa hatua za kisheria huku Akisisitiza kuwa vyombo vya usalama vitaendelea kuwabaini na kuwakamata wote watakaotumia maandamano hayo kama fursa ya kufanya uhalifu.
Maandamano hayo yamechochewa na makundi yanayopinga uhamiaji haramu, ambayo yalitangaza Juni 30 kuwa muda wa mwisho kwa wahamiaji wasiokuwa na vibali kuondoka nchini. Makundi hayo yanadai wahamiaji hao wamechangia kuongezeka kwa ukosefu wa ajira kwa kukubali mishahara midogo pamoja na kuhusishwa na ongezeko la uhalifu na changamoto nyingine za kijamii.
Hata hivyo, serikali ya Afrika Kusini imekataa kutambua muda huo wa mwisho, ikisisitiza kuwa ni serikali pekee yenye mamlaka ya kusimamia na kutekeleza sheria za uhamiaji.






