Umoja wa Mataifa (UN) umetangaza kuwa utafunga rasmi Ofisi yake ya Haki za Binadamu nchini Burkina Faso baada ya utawala wa kijeshi kusimamisha kwa muda usiojulikana shughuli za ofisi hiyo, hali iliyoifanya ishindwe kuendelea kutekeleza majukumu yake nchini humo.
Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesema uamuzi huo umetokana na hatua ya mamlaka ya kijeshi kusitisha operesheni za ofisi hiyo, jambo lililozuia shughuli zake za kulinda na kutetea haki za binadamu.
Hatua hiyo imekuja miezi mitatu baada ya serikali ya kijeshi ya Burkina Faso kusimamisha shughuli za ofisi hiyo kufuatia taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyozitaka mamlaka kuheshimu haki za binadamu na kulinda nafasi ya kiraia.
Ofisi hiyo, iliyofunguliwa mwezi Oktoba 2021, inatarajiwa kufungwa rasmi ifikapo Novemba 30 mwaka huu.
Katika kipindi cha uendeshaji wake, ilifanya ufuatiliaji na uchunguzi wa masuala ya haki za binadamu, pamoja na kutoa mafunzo kwa takriban maafisa 4,000 wa vikosi vya ulinzi na usalama kuhusu sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kibinadamu.
Tangu Ibrahim Traoré achukue madaraka kupitia mapinduzi ya Septemba 2022, serikali ya kijeshi imekuwa ikifuata sera zinazopinga ushawishi wa mataifa ya Magharibi, huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakionyesha wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ukandamizaji dhidi ya wakosoaji wa serikali.






