Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amewasili mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa ziara fupi ya kikazi inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika maandalizi, kinga na mwitikio dhidi ya milipuko ya magonjwa barani Afrika.

Ziara hiyo imefanyika katika nafasi yake kama Bingwa wa Umoja wa Afrika (AU) wa Ajenda ya Maandalizi, Kinga na Mwitikio wa Magonjwa ya Mlipuko. Jukumu hilo linahusisha kuhamasisha nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano katika mifumo ya afya, utafiti wa kisayansi na uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N’djili, Ramaphosa alipokelewa na Waziri Mkuu wa DRC, Judith Suminwa, kabla ya kuelekea katika makao ya Umoja wa Afrika mjini Kinshasa kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Rais wa DRC, Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo.

Mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan kujenga uwezo wa bara kujitegemea katika utafiti wa kisayansi, ufuatiliaji wa magonjwa na utoaji wa huduma za afya wakati wa dharura.

Baada ya mkutano huo, viongozi hao walitembelea Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba (INRB), ambayo imekuwa mstari wa mbele katika utafiti na mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko, ikiwemo Ebola nchini DRC.

Ziara hiyo pia iliwapa fursa ya kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika utafiti wa kisayansi, uchunguzi wa maabara na mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa.
Aidha, viongozi hao walizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kuimarisha sekta ya afya, ili Afrika iweze kukabiliana na milipuko ya magonjwa kwa ufanisi zaidi bila kutegemea misaada ya nje pekee.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, jumuiya ya kimataifa imeahidi zaidi ya dola za Marekani milioni 910 kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola nchini DRC. Kati ya fedha hizo, Afrika Kusini imechangia dola milioni 13.5, hatua inayodhihirisha mshikamano wa nchi hiyo katika kuunga mkono juhudi za kudhibiti milipuko ya magonjwa na kuimarisha usalama wa afya barani Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here