Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameliagiza Jeshi la Israel kuongeza mashambulizi na kuharibu miundombinu yote ya kundi la Hezbollah katika eneo la kusini mwa Lebanon.
Akiwa katika ziara ya kuwatembelea wanajeshi wa Israel, Netanyahu alisema operesheni hiyo inalenga kuharibu miundombinu yote ya Hezbollah, iwe iliyopo juu ya ardhi au chini ya ardhi, ikiwemo mtandao wa mahandaki unaodaiwa kutumika kutekeleza mashambulizi dhidi ya Israel.
Netanyahu amesisitiza kuwa Jeshi la Israel halitaondoka katika maeneo ya mpakani hadi Hezbollah itakapoweka chini silaha na kutokuwa tena tishio kwa usalama wa Israel. Aidha, alidai kuwa operesheni hizo za kijeshi zimepunguza kwa kiwango kikubwa uwezo wa kijeshi wa kundi hilo.
Kwa upande mwingine, Serikali ya Lebanon pamoja na Hezbollah zimekosoa vikali hatua hiyo, zikisema kuwa eneo la usalama lililoanzishwa na Israel kusini mwa Lebanon ni uvamizi unaokiuka sheria za kimataifa.
Hezbollah ni kundi linaloungwa mkono na Iran. Kwa mujibu wa makadirio yaliyoripotiwa na vyombo vya habari vya Lebanon, eneo linalodhibitiwa na Israel kusini mwa Lebanon lina ukubwa wa takriban kilomita za mraba 620, sawa na karibu asilimia 6 ya eneo lote la Lebanon.






