Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema wananchi wa mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi wanahitaji huduma za meli ya MV Liemba kwa shughuli za kiuchumi na kijamii, hivyo amewataka wasimamizi wa mradi wa ukarabati kuhakikisha meli hiyo inaanza kutoa huduma ifikapo mwisho wa Julai.

Profesa Mbarawa amesema hayo wakati wa ziara yake katika Bandari ya Kigoma, alikokwenda kukagua maendeleo ya maboresho ya miundombinu ya bandari pamoja na ukarabati wa MV Liemba.

Amesema taarifa alizopokea zinaonyesha kuwa ukarabati wa meli hiyo umefikia asilimia 90, hivyo amesisitiza kuwa asilimia 10 iliyobaki ikamilishwe kwa wakati ili meli ianze kutoa huduma mwezi Julai.

Waziri Mbarawa amesema amezungumza na wahandisi pamoja na wasimamizi wa mradi huo ili kufahamu iwapo kuna changamoto zinazohitaji ufumbuzi kutoka serikalini.

Amesema wamehakikisha kuwa hakuna changamoto zinazoweza kuchelewesha kukamilika kwa mradi huo.

“Kwetu sisi, meli hii ni muhimu kwa maisha ya wananchi wanaoishi kandokando ya Ziwa Tanganyika. Imekuwa nguzo ya shughuli za kiuchumi na usafiri. Tunaitaka irejee kutoa huduma haraka, kwani itachangia kutekeleza azma ya Serikali ya kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha biashara na uchumi,” alisema Profesa Mbarawa.

Awali, Meneja wa Mradi wa Ukarabati wa MV Liemba, Mhandisi Elius Kivara, alisema ukarabati wa meli hiyo unagharimu shilingi bilioni 33 na umefikia asilimia 90.

Alisema kuwa kuanzia Julai 15 mwaka huu, wataanza kufanya majaribio ya meli hiyo baada ya kukamilisha ufungaji wa injini mpya pamoja na vifaa vingine katika maeneo mbalimbali ya meli.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here