Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limebaini kuwa Ramadhan Jafari maarufu kwa jina la Muna (47), ambaye aliripotiwa kupotea, aliuawa na kufukiwa ndani ya nyumba yake katika eneo la Mbezi Luguruni Kwembe, Wilaya ya Ubungo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema taarifa za kupotea kwa marehemu zilipokelewa Juni 16, 2026 katika Kituo cha Polisi Kimara Gogoni, na uchunguzi uliofanyika baadaye ulibaini kuwa aliuawa na kufukiwa ndani ya moja ya vyumba vya nyumba yake.

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, uchunguzi huo uliwezesha kukamatwa kwa mtoto wa marehemu, Juma Ramadhan maarufu kwa jina la Juli (21), katika eneo la Msufini, Msoga mkoani Pwani, ambaye anadaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Polisi wamesema mtuhumiwa alieleza namna alivyomuua baba yake na kufukia mwili wake ndani ya nyumba, huku sababu za tukio hilo zikiendelea kuchunguzwa.

Jeshi la Polisi limelaani vikali tukio hilo na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama katika kuzuia na kufichua uhalifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here