Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU ), mkoa wa Mwanza imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 100, fedha ambayo ilikuwa mali ya Chama cha Ushirika cha Bukasiga kilichopo Wilayani Ukerewe mkoani humo.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza Mhandisi Abnery Mganga, akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 17, 2026 amesema walipokea malalamiko kutoka kwenye chama hicho kinachojishughulisha na shughuli za uvuvi, ikielezwa kwamba viongozi wa chama hicho walichukua mkopo wa Sh.milioni 106 katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ( TADB ) kwa ajili ya ujenzi wa kaushio la dagaa na kuzitoa fedha hizo kwa kampuni ya SUGECO kwa ajili ya ujenzi wa kaushio hilo.
Aidha bosi huyo wa TAKUKURU Mwanza amesema wanachama wa chama hicho cha ushirika cha Bukasiga walidai kwamba kampuni hiyo ilijenga kaushio ambalo halikidhi mahitaji ambapo lilifanya kazi kwa muda mfupi na kuungua huku wana ushirika hao wakijikuta wanalipa mkopo ambao hawana manufaa nao.
Mganga ameongeza kuwa baada ya taarifa hiyo kufika TAKUKURU walifanya uchunguzi wa kina na kampuni ilikiri kufanya kazi chini ya kiwango hivyo kulazimika kurejesha fedha hizo kiasi cha zaidi ya shilingi milioni mia moja.
TAKUKURU imetoa wito kwa vyama vya ushirika kuchagua uadilifu katika shughuli zao wanazofanya kufuatia vyama hivyo kuanzisha kampeni inayojulikana kama “chagua uadilifu, linda ushirika” iliyozinduliwa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza Said Mtanda.







