Chuo Kikuu cha RUDN cha nchini Urusi, maarufu kama Patrice Lumumba kimemtunuku Rais Samia Suluhu Hassan Shahada ya Uzamivu ya Heshima (Honoris Causa) kwa kutambua mchango wake katika uongozi bora, diplomasia na maendeleo ya jamii.

Tuzo hiyo imetolewa wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais Samia nchini Urusi, ambapo amekuwa akifanya mazungumzo yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Urusi.

Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Rais Samia amesema heshima hiyo ni kubwa kwake binafsi na kwa Taifa la Tanzania kwa ujumla, akieleza kuwa ni ishara ya kutambuliwa kwa mchango wa nchi katika maendeleo na ushirikiano wa kimataifa.

Rais Samia amesema dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu ili kuharakisha maendeleo endelevu.

Aidha amefafanua kuwa wataalamu waliobobea katika nyanja mbalimbali ni nguzo muhimu katika kujenga uchumi imara na wenye ushindani, huku maarifa na ubunifu vikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa.

Hatahivyo Rais Samia amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta za elimu, utafiti na teknolojia ili kuwawezesha vijana kupata maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la kimataifa pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here