Ndoto ya Serengeti Boys kutwaa taji lao la kwanza la Afrika imegonga mwamba baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penati 4-2 na Senegal katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) iliyopigwa mjini Rabat, Morocco.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 kabla ya Senegal kuonyesha utulivu mkubwa katika mikwaju ya penati na kutwaa ubingwa wao wa pili wa mashindano hayo ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Tanzania ilianza fainali hiyo kwa nguvu na kuwatikisa mabingwa wa mwaka 2023 mapema kabisa. Dakika ya saba, Hamis Chenga aliifungia Serengeti Boys bao la kuongoza baada ya kumalizia vyema shambulizi lililoanzia katikati ya uwanja, na kuwapa matumaini makubwa mashabiki wa Tanzania kwamba historia mpya ilikuwa karibu kuandikwa.

Hata hivyo, Senegal walionyesha uzoefu na ubora wao kwa kutawala sehemu kubwa ya mchezo. Juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 64 wakati Ibrahima Dione alipotumia vyema mpira wa adhabu uliopigwa na Souleymane Faye na kusawazisha mchezo baada ya kipa wa Tanzania, Haji Abdallah, kushindwa kuudhibiti mpira huo.

Baada ya bao hilo, mchezo ulizidi kuwa wa ushindani mkubwa huku kila timu ikisaka bao la ushindi. Serengeti Boys waliendelea kupambana kwa nidhamu na uthabiti mkubwa, wakionesha moyo ule ule uliowavusha katika robo fainali dhidi ya Algeria na nusu fainali dhidi ya Misri.

Hata hivyo, baada ya sare ya 1-1 kudumu hadi mwisho wa muda wa kawaida, mshindi aliamuliwa kwa mikwaju ya penati. Senegal walikuwa wakamilifu kwa kufunga penati zao zote nne, huku Tanzania ikishindwa kutumia nafasi mbili muhimu, jambo lililoifanya ndoto ya ubingwa kuyeyuka dakika za mwisho.

Licha ya kupoteza fainali, Serengeti Boys wameondoka Morocco wakiwa na mafanikio makubwa ya kihistoria. Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufika fainali ya AFCON U-17 na mara ya kwanza kwa timu ya taifa ya Tanzania kufika hatua hiyo katika mashindano makubwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Katika safari yao ya kuvutia, Tanzania ilimaliza kinara wa Kundi C kwa kuwashinda Msumbiji na Angola kabla ya kupoteza dhidi ya Uganda. Katika hatua za mtoano, Serengeti Boys walionesha uimara wa kiakili kwa kuziondoa Algeria na Misri kupitia mikwaju ya penati.

Zaidi ya yote, safari hiyo imeihakikishia Tanzania tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la FIFA la vijana chini ya miaka 17, mafanikio makubwa yanayodhihirisha ukuaji wa soka la vijana nchini na kuipa taifa matumaini makubwa ya siku zijazo.

Ingawa taji limeenda Senegal, Serengeti Boys wameondoka Morocco wakiwa mashujaa na wameweka msingi mpya wa mafanikio ya soka la Tanzania katika ngazi ya kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here