Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewaalika wakazi wa mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushuhudia na kuipa sapoti timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, itakayocheza fainali dhidi ya Senegal hapo kesho.

Mtanda amesema maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya kuonyesha mchezo huo kupitia skrini kubwa itakayowekwa katika Uwanja wa ROCK CITY jijini Mwanza, ambapo wananchi watapata fursa ya kuutazama mchezo huo kwa pamoja huku wakiipa hamasa timu yao.

Mbali na maandalizi hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema zawadi maalum zitatolewa kwa wananchi watakaobuni na kusambaza maudhui bora ya kuhamasisha ushindi wa Serengeti Boys kupitia mitandao ya kijamii katika kipindi hiki cha kuelekea fainali.

Amesema lengo la hatua hiyo ni kuendelea kuhamasisha uzalendo na mshikamano wa Watanzania katika kuisapoti timu hiyo ambayo imeonyesha kiwango kizuri na kufanikiwa kutinga hatua ya fainali ya mashindano hayo.

Hamasa hiyo jijini Mwanza inakuja kufuatia kauli ya Waziri wa Michezo Paul Christian Makonda, alipotoa wito kwa mikoa yote nchini kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wananchi kushuhudia mchezo huo kwa pamoja kupitia skrini kubwa na shughuli mbalimbali za kuhamasisha sapoti kwa Serengeti Boys.

Serengeti Boys inatarajiwa kushuka dimbani siku ya kesho kuvaana na Senegal katika mchezo wa fainali unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, huku Watanzania wakitarajia kuona vijana hao wakiiandikia historia mpya Tanzania katika soka la vijana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here