TAIPEI, Taiwan
CHINA na Taiwan ziko jirani, zikitenganishwa na Mlango-Bahari tu. Kwa miaka mingi sasa, pande mbili hizo zimekuwa kwenye mgogoro wa kisiasa unaotishia kuziingiza vitani.
Chanzo ni madai ya China, kwamba Kisiwa hicho ni sehemu ya ardhi yake, hivyo umefika wakati wa kukiunganisha na eneo la bara. Wanaitafsiri Taiwan kama jimbo tu.
Mara kadhaa mamlaka za China zimenukuliwa zikidai kuwa mchakato wa kuidhibiti Taiwan utafanyika aidha kwa amani au nguvu kama itabidi.
Kwa Taiwan, ambayo ina watu milioni 23 na Serikali yake iliyochaguliwa kidemokrasia, imeendelea kusisitiza kuwa Kisiwa hicho ni nchi yenye mamlaka kamili.
Wakati China ikitishia mara kadhaa kuwa itaivamia kijeshi Taiwan, wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema Marekani haitokaa kimya, na badala yake itaingia vitani kukisaidia Kisiwa hicho.
CHANZO CHA MGOGORO
Katika karne ya 20, China iliingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Serikali ya Rais Chiang Kai-shek na wanaharati wa ujamaa wakiongozwa na Mao Zedong.
Wakati huo, Marekani ilikuwa ikiiunga mkono Serikali iliyokuwa madarakani. Vita vikipokwisha na ujamaa kushinda, viongozi wa Kibepari walikimbilia Kisiwa jirani cha Taiwan, ambako waliunda Serikali yao.
Hata hivyo, Chama cha Ujamaa cha China (CCP) kiliendelea kutokuitambua Taiwan kama nchi, na badala yake kukitaja Kisiwa hicho kuwa ni eneo lililoko chini ya mamlaka yake.
Mwaka 2024, baada ya ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu, Rais wa Taiwan, Lai Ching-te, alisema wanaikaribisha China kwa mazungumzo ya kumaliza mgogoro lakini kwa sharti la Taifa lake kuheshimiwa na kutambulika kama mamlaka kamili.
SURA YA TAIWAN KIMATAIFA
Kwa sasa, Taiwan si mwanachama rasmi wa Umoja wa Mataifa (UN) lakini ina hadhi ya nchi katika taasisi za kimataifa zaidi ya 40, zikiwamo Benki ya Maendeleo ya Asia na Shirika la Biashara la Kimataifa.
Ni mataifa 11 pekee duniani yenye uhusiano wa kidiplomasia na Taiwan. Machi, 2023, Honduras ilisitisha uhusiano na Kisiwa hicho na kuimarisha uhusiano wake na China.
PRESHA KWA TAIWAN
China imefanya mambo kadhaa kuilazimisha Taiwan kusalimu amri. Mwaka 2016, ilizitaka kampuni za utalii za kimataifa kuitambua Taiwan kama jimbo la China na si kuwasiliana nayo moja kwa moja kama nchi.
Presha nyingine waliyoiweka China ni kuzifungia mlango wa kibiashara nchi zote zinazoshirikiana na Taiwan, kama ilivyofanya kwa Lithuania.
CHINA KUFUATA NYAYO ZA URUSI?
Baada ya Urusi kuwavamia majirani zao, Ukraine, mwaka 2022, ilizuka hofu kwamba huenda China nayo ingechukua hatua hiyo kwa Taiwan.
Hisia za aina hiyo zilijitokeza tena Januari, 2026, baada ya wanajeshi wa Marekani kuivamia Venezuela na kumnyakua Rais aliyekuwa madarakani, Nicolas Maduro.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, Taiwan itahitaji msaada wa nje, hasa kutoka Marekan, ili kumudu vita endapo itavamiwa na China.
Licha ya kutumia Dola bilioni 20 katika ulinzi mwaka 2025, China imetumia mara 11 ya kiasi hicho Cha fedha kuwekeza kwenye ulinzi.
MAREKANI KUINGILIA KATI?
Kwa miaka mingi, Marekani imekuwa ikiiunga mkono Taiwan. Katika awamu ya kwanza ya urais wake, Donald Trump aliiuzia Taiwan silaha za kivita zenye thamani ya Dola bilioni 18.
Wakati huo huo, Rais Trump aliidhinisha Dola milioni 250 zilizotumika kujenga ubalozi wa Marekani wake Taiwan, sambamba na kukutana mara kwa mara na viongozi wa Serikali ya Kisiwa hicho.
Hatua kubwa zaidi ni ile ya Joe Biden, ambaye alikuwa Rais wa kwanza wa Marekani kuwaalika wawakilishi wa Taiwan katika hafla ya kuapishwa kwake.
Bunge la Marekani lilipitisha muswada uliosainiwa na Rais Biden kuiruhusu Taiwan kupata mkopo wa silaha wa hadi Dola bilioni moja kwa mwaka.
Hata hivyo, unafuu huo wa Taiwan umepungua tangu Rais Trump aliporejea madarakani. Utawala wake umeziwekea ushuru wa asilimia 15 bidhaa zote zinazotoka Taiwan na China.
Licha ya kwamba Rais Trump hajaweka wazi kama Marekani itaisaidia Taiwan endapo itavamiwa na China, wachambuzi wa siasa wanaliona hilo likitokea.
WANANCHI WA TAIWAN WANASEMAJE?
Tafiti nyingi zinaonesha kuwa wanataka Taiwan yao itambulike kuwa ni nchi huru, badala ya kuwa sehemu ya China. Utafiti wa Chuo Kikuu cha Chengchi wa mwaka 2023 ulibaini kuwa asilimia 63 wanataka uhuru.






