SIMBA v YANGA: DAKIKA 90 ZA KISASI, HESHIMA LIGI KUU BARA WIKIENDI HII

Date:

Share post:

EBWANA ee! Hebu sahau kidogo kile kilichotokea siku chache zilizopita katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ambako Simba iiifunga Yanga bao 1-0 na kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano.

Jumapili ya wiki hii, Mei 3, 2026, vigogo hao wa soka la Tanzania wataoneshana tena kazi katika dakika 90 za ‘derby’ ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo.

MECHI YA KISASI
Yanga wakiwa wageni wa mchezo, watashuka dimbani wikiendi hii wakiwa hawajasahau maumivu waliyoachiwa na Simba katika mchezo wa Jumatano ya wiki hii, Aprili 29, 2026.

Ukiwa ni mtanange wa fainali ya Kombe la Muungano, timu hizo zikiwa zimebakiza sekunde chache kumaliza dakika 120 (90 + 30), Clatous Chama alisababisha penalti baada ya kuchezewa rafu ndani ya boksi la Yanga.

Seleman Mwalim alipiga mkwaju huo wa penalti na kufunga bao pekee hilo lililozamisha jahazi la Yanga na kuipa Simba ubingwa wake wa saba wa michuano hiyo.

Hivyo, wakati Yanga wakiiona mechi ya wikiendi hii ni nafasi ya kulipiza kisasi kwa kile walichofanyiwa Visiwani Zanzibar, Simba watatamani kutonesha kidonda cha wapinzani wao hao. Patamu hapo!

VITA YA KILELENI MWA MSIMAMO
Achilia mbali ishu ya kisasi, timu hizo zinakutana katika wakati ambao zinapeana presha kubwa katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Kila moja imeshacheza mechi 19 na Yanga ‘Timu ya Wananchi’ wako kileleni wakiwa na pointi 47, wakiizidi tano tu Simba inayoshika nafasi ya pili.

Hivyo, endapo ‘Wekundu wa Msimbazi’ watashinda wikiendi hii, watabakiza pointi mbili pekee kuifikia Yanga. Kinyume chake, Yanga wakishinda wataongeza pengo la pointi na kufikia nane.

MWENDO WA MABAO TU
Katika mechi 19 walizoshuka dimbani msimu huu, mabingwa watetezi msimu huu wa Ligi Kuu Bara, Yanga, wameshinda 14 na kutoa sare tano.

Mechi hizo zimeishuhudia Yanga ikiongoza kwa upachikaji mabao (44), pia ikiwa ndiyo timu iliyoruhusu nyavu zake kutikiswa mara chache zaidi (3).

Kwa upande wa Simba, katika michezo 19 waliyocheza kufikia hatua hii ya msimu wa Ligi, wameshinda 12, sare sita na kufungwa mmoja.

Simba, kwa upande wao, wameshafunga mabao 32, huku safu ya ulinzi ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba pekee.

SOMA HAPA
Vigogo hao wa Ligi Kuu Bara, Yanga na Simba, watakutana kwa mara ya pili msimu huu wa Ligi Kuu Bara baada ya matokeo ya suluhu (0-0) katika mchezo wa kwanza.

Kwamba timu itakayoshinda wikiendi hii, itajivunia kumaliza msimu huu ikiwa imezoa pointi nne za mpinzani wake. Je, ni Simba au ni Yanga? Tusubiri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

NAMIBIA YA MALIZA DENI LA IMF

Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, ameiongoza nchi yake kufikia hatua muhimu ya kiuchumi baada ya kukamilisha malipo yote...

SERIKALI KUONGEZA UWEKEZAJI KWA WAKUNGA KUIMARISHA AFYA YA MAMA NA MTOTO NCHINI

Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuendelea kuongeza uwekezaji katika mafunzo, ajira, motisha na mazingira ya kazi kwa...

POLISI KUENDELEA KUDHIBITI WAZUSHI MITANDAONI, LIKIIMARISHA ULINZI KUELEKEA DERBY YA SIMBA NA YANGA

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa taarifa ya matukio mbalimbali ya kiusalama na kisheria,...

DKT. SAMIA AFANYA UTEUZI, UTENGUZI NA UHAMISHO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi na uhamisho wa baadhi...