Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuendelea kuongeza uwekezaji katika mafunzo, ajira, motisha na mazingira ya kazi kwa wakunga kwa lengo la kuzidi kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.
Hayo yamesema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe leo Mei 2, 2026 wakati akizungumza katika Maadhimisho ya siku ya Mkunga Duniani iliyofanyika Mkoani Kilimanjaro, Ambapo ametoa wito kwa wakunga wote nchini kuendelea kutoa huduma za afya kwa weledi, juhudi na kuzingatia maadili ya taaluma zao ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto unaimarika.
Aidha ameongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokiuka maadili ya taaluma huku akisisitiza kuwa, Serikali haitasita kuwawajibisha watoa huduma watakaotoa huduma kinyume na viwango vinavyotakiwa, ili kulinda hadhi ya taaluma na usalama wa wagonjwa.
Sanjari na hayo Dkt. Shekalaghe ameihimiza jamii kutumia huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya ili kupata huduma sahihi kutoka kwa wakunga wataalamu badala ya kujifungulia nyumbani bila uangalizi wa kitaalamu huku akihimiza ushirikiano kati ya jamii na watoa huduma ni muhimu hasa wakati wa dharura, kwani huongeza uwezekano wa kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Katika hatua nyingine, Dkt. Shekalaghe ameitaka jamii kuwaunga mkono wakunga kwa kuwaheshimu, kushirikiana nao na kuhakikisha wanapata huduma za afya mapema na kwa wakati.
“Serikali inatambua mchango wenu wakunga kwa kazi kubwa mnayoifanya, Tuzo aliyotunukiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ‘Goalkeeper’ kama kinara wa kupunguza vifo vya mama na mtoto, lakini pia kuchaguliwa kwake kuwa Kinara wa masuala ya mama na mtoto Afrika, ni dhahiri ya juhudi na utendaji kazi wenu bora, hivyo nawapongeza sana” amesema Dkt. Shekalaghe
Hatahivyo, Dkt. Shekalaghe amesisitiza kuwa, wadau wa sekta ya afya kushiriki kikamilifu katika kuboresha huduma za afya ya uzazi na kuweka mazingira bora yatakayowawezesha wakunga kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.






