Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi na uhamisho wa baadhi ya viongozi wa serikali katika wizara mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 2, 2026 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Mhe. Dkt. Evaline Wilbard Munisi (Mb.) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano. Anachukua nafasi ya Mhe. Rahma Riyadh Kisau (Mb.) ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Katika mabadiliko hayo, Bw. Eliakim Chacha Maswi amehamishwa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Aidha, Dkt. John Antony Jingu amehamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari S. Machumu.







