Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa taarifa ya matukio mbalimbali ya kiusalama na kisheria, ikiwemo hukumu ya kesi ya mauaji, kukamatwa kwa watuhumiwa wa taarifa za uongo mitandaoni pamoja na maandalizi ya ulinzi kuelekea mchezo mkubwa wa ligi kuu.
Katika tukio la kwanza, Polisi imeeleza kuwa Aprili 30, 2026, Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam (Masijala Ndogo) ilimhukumu kunyongwa hadi kufa Abdalah Mussa maarufu kama Mr. Blue, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi aliyekuwa mpenzi wake, Ezenia Kamana.
Tukio hilo lilitokea Agosti 19, 2024 katika eneo la Chang’ombe Maduka Mawili, Wilaya ya Temeke, ambapo mwili wa marehemu ulipatikana ukiwa umekatwakatwa na kutupwa katika maeneo ya Ununio, Kunduchi na Tegeta, wilayani Kinondoni.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi limewakamata watu wanaodaiwa kuhusika na kusambaza taarifa za uongo mitandaoni, akiwemo Mocrine Julius maarufu kama mazidi mkazi wa Salasala, Kinondoni. Watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa tuhuma za kueneza taarifa zilizolenga kuleta taharuki katika jamii.
Katika hatua nyingine, Polisi imetangaza kuimarisha ulinzi kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba SC na Yanga SC utakaochezwa Mei 3, 2026 kuanzia saa 12:00 jioni katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo. Jeshi hilo limewataka mashabiki na wadau wa soka kuzingatia amani, nidhamu na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga utaratibu wa mchezo huo.






