Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Amos Gabriel Makalla, Mei Mosi 2026 amewataka waajiri kuhakikisha wanawasilisha kwa wakati michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii kwa mujibu wa sheria za nchi.
Akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Mhe. Makalla pia alisisitiza umuhimu wa wafanyakazi kuwajibika kazini ili wawe na msingi imara wa kudai haki zao.
Aidha, amehimiza uadilifu na ushirikiano mzuri kati ya waajiri na wafanyakazi, pamoja na kubainisha kuwa hali hiyo ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla huku akikemea vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya huduma za kijamii na kuagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya watakaobainika kufanya vitendo hivyo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Makalla amewataka wananchi wa Arusha kujipanga kunufaika na ujio wa mkutano wa kimataifa wa Bunge la Dunia (IPU), unaotarajiwa kufanyika Oktoba 3 hadi 10, 2026 katika Arusha International Conference Centre (AICC).
Amesema zaidi ya wajumbe 3,000 wanatarajiwa kushiriki mkutano huo, hivyo ni fursa kubwa kwa wakazi wa Arusha, hususan katika sekta za biashara, usafiri, utalii na huduma za malazi.
“Aliyepo sokoni atafaidika kwa sababu hoteli zitanunua bidhaa kwa ajili ya vyakula, mwenye usafiri atafaidika na mwenye hoteli naye atafaidika. Huu ni mnyororo wa thamani utakaomgusa kila mtu,” amesema Makalla.
Mbali na hayo Makalla ameongeza kuwa wageni wengi watakaohudhuria watakuja pia na familia zao na huenda wakatenga muda wa kutembelea vivutio vya utalii, hivyo kutoa wito kwa wadau wa sekta hiyo na wafanyakazi kwa ujumla kutoa huduma bora ili kuendelea kuitangaza Tanzania kama nchi salama na yenye kuvutia kwa uwekezaji na utalii.






