Wednesday, June 25, 2025
spot_img

RAIS SAMIA- DUNIA SASA INAKABIRIWA NA CHANGAMOTO KUBWA MBILI

RAIS Samia Suluhu Hassan akiwa nje ya ukumbi wa mikutano wa Umoja wa Mataifa (UN), ulioko New York, Marekani baada ya kushiriki mkutano uliojadili mabadiliko ya tabianchi duniani. Kulia ni Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Liberata Mulamula na kushoto ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Kennedy Gaston  

 

MWANDISHI WA PANORAMA

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema dunia inakabiriwa na changamoto za aina mbili kwa wakati mmoja, huku moja ikisababisha kuanguka kwa uchumi na kufuta mafanikio yaliyofikiwa na jamii nyingi katika miongo kadhaa.

 

Akizungumza jana jijini New York, Marekani kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa uliojadili athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia, alisema wakati dunia inapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, inalazimika pia kukabiliana na changamoto nyingine kubwa ambayo ugonjwa wa virusi vya Corona.

 

Rais Samia alisema dunia haipaswi kupuuza juhudi za kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi ingawa watu wengi hawaonyeshi kushtushwa na kupanda kwa hali ya joto duniani kama moja ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

 

Alisema hali ni ya kusikitisha kwa nchi kama Tanzania ambayo mabadiliko ya tabianchi yanasababisha ukame ambao una athari mbaya kwa sekta zinazotegemea maliasili kama vile kilimo, uvuvi na misitu zinazochangia asilimia 30 ya pato la taifa na kuathiri takriban asilimia 60 ya watu.

 

Rais Samia na viongozi wa mataifa mengine duniani walishiriki mkutano huo ambao ni mfululizo wa mikutano ya maandalizi ya mkutano mkuu wa 26 wa athari za mabadiliko ya tabianchi (COP26) unatarajiwa kufanyika Glasgow, Uskochi, Novemba 2021.

 

Mkutano huo pia ulijadili jinsi ya kupatikana kwa fedha za kugharamia ustahimilivu wa upunguzaji wa athari za mabadiliko ya tabianchi duniani.

 

Ajanda nyingine katika mkutano huo ilikuwa umuhimu wa kutilia mkazo hatua za mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia ambayo athari zake ni pamoja na uharibifu wa mazingira unaosababisha kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi na kuhatarisha usalama wa nchi.

 

Kauli mbiu ya mkutano huo ambao ni moja wa mikutano mahususi ya kilele kuelekea mkutano mkuu wa 76 wa Umoja wa Mataifa ni ‘kujenga ustahimilivu kupitia matumaini- kuondokana na UVIKO 19, kufanyia kazi mahitaji ya ulimwengu, kuheshimu haki za watu na kuboresha Umoja wa Mataifa.’

 

Wakati huo huo, Rais Samia amekutana na Rais wa Comoro, Azali Asoumani na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Rebecca Nyandeng Garang.

 

Katika mazungumzo yake na viongozi hao, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano na alielekeza kufanyika haraka kwa mikutano ya tume za kudumu za ushirikiano baina ya Tanzania na mataifa hayo.

 

Aidha, Rais Samia alikutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), Filippo Grand na kukubaliana kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na shirika hilo, hasa kusaidia wakimbizi walioko Tanzania.


RAIS Samia Suluhu Hassan akitoka katika mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN)  uliojadili mabadiliko ya tabianchi duniani.


 

  

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya