Tuesday, December 24, 2024
spot_img

ROHO IMEKUFA MWILI UNAISHI

 
Mullinda
NIMEFIKISHIWA ujumbe wa kienyeji kuwa watu wanaojeruhi wenzao kwa vitu vyenye ncha kali hawafurahishwi na maandishi yangu.
Ujumbe huo niliofikishiwa unaeleza kuwa maandishi yangu yanawaudhi wenye roho na miili ya kinyama wanaoishi katikati ya miili yenye roho zilizokufa.
Hawayapendi kwa sababu yanawaudhi, wanayasoma kwa kujilazimisha kwa sababu yanavutia kusomwa lakini yanaudhi yanaposomwa. Wamekasirika.
Maandishi yangu yanawafikirisha hadi uwezo wao wa mwisho wa kufikiri.
Kwa sababu mwisho wa uwezo wao wa kufikiri ni kujeruhi wenzao kwa vitu vyenye ncha kali, nadhani hata katika hili inaweza kuwa hivyo.
Mungu apishilie mbali kwa sababu mwili umeumbwa kwa udongo uliogeuzwa kuwa nyama. Nyama husikia maumivu makali inapotobolewa hovyo hovyo na kitu chenye ncha kali hivyo ikitokea nikatobolewa tobolewa bila mpangilio, nitaumia sana.
Mwili wangu ni bora zaidi kuliko roho ambayo iko ndani ya mwili wangu ikiwa ilishakufa hivyo nina wajibu wa kuulinda mwili usitobolewe na vitu vyenye ncha kali.
Ndiyo tegemeo langu pekee lililobaki linaloniwezesha kuwepo duniani. Ni mwili tu, siyo roho ambayo ilishakufa kitambo kutokana na ukakasi wa maisha.
Hivyo, kwa yeyote mwenye mawazo ya kujeruhi mwili wangu, kama kweli yupo, namshauri asifanye hivyo, anachopaswa kufanya ni kuichukua tu roho yangu. Akifanya hivyo atakuwa amenisaidia sana kuepukana na maisha magumu yaliyowezekana.
Hakuna haja ya kudadisi mwenendo wa maisha yangu kwa sababu unafahamika. Ninaishi maisha ya kichokonozi, ninapatikana kwa urahisi sana kwa sababu sijifichi, maeneo ninayopendelea kufika ni vilabuni na kwenye nyumba za wageni, sina makazi maalumu hivyo yeyote mwenye nia ya kunifikia anaweza, tena kwa urahisi sana.
Sina akili ya kujificha kwa sababu roho imekufa. Bila roho nadhani hakuna akili ila akili na roho vinaweza kuwa vimekufa lakini mwili ukawa unaishi.
Hivyo ndivyo ilivyo kwangu, niko tofauti sana na waliokufa miili na roho ambao walijaribu kukikimbia kifo lakini kiliwafuata huko huko, kikawaua.
Hawa ni wale waliotamani vyote bila kujua kuwa mtaka vyote hukosa vyote. Waliutamani utwana na ubwana kwa wakati mmoja, maneno yao yalikuwa ya kitwana huku vitendo vyao vikiwa vya kibwana, walipogutuka wakajikuta wametengwa peke yao, wakaachwa wafe kivyao.
Walijaribu wengi kukikimbia kifo cha roho na mwili, tena walikimbilia kwa wazungu lakini ziraili mnyotoa roho hakuwaacha, aliwafuata na kuwaua. Heri wangekubali kufa nusu na wakabaki na uhai nusu, yaani wangeruhusu kifo cha roho ili kunusuru mwili.
Mwili usiokuwa na roho ni mwili mpweke na kwa sababu ya upweke huo, ukionewa kwa bahati mbaya au makusudi hukasirika, ukikasirika hufanya lolote kwa sababu huhisi unaonewa kwa vile ni mpweke.
Ndiyo maana alipojitokeza punguani mmoja na kuusononesha mwili wangu kwa kudhihaki mtu ninayempenda mno ambaye ni mgonjwa, punguaji huyo nilimkemea kwa kumpa sifa anayostahili ambayo  ni ujinga na yeye mwenyewe alikubaliana na sifa hiyo kwa sababu alibaini kuwa kweli ni mjinga.
kitu chenye ncha kali
Mtu yeyote mwenye mwili ulioumbwa kwa udongo uliogeuzwa kuwa nyama anapomuona mtu aliyeumbwa kwa mfano wake akiwa ametobolewa tobolewa mwili wake kikatili, akiwa amepondwapondwa na kuvunjwa vunjwa viungo vyake kinyama ni lazima atayahisi maumivu ya ukatili huo ambao haupaswi kufanywa na binadamu mwenye mwili pekee isipokuwa binadamu mwenye mwili na roho ya kinyama, anayeishi katikati ya miili mingi isiyokuwa na roho inayoishi katika mashaka na hudhuni kubwa ya kukosa mtetezi.
Watanzania wengi roho zao zimekataa tama. Wamekata tamaa ya maisha, wanaishi maisha ya bora liende, hawajui kesho yao, wapo wapo tu. Kwa lugha ya kichokonozi hawa ndiyo wale ambao roho zao zimekufa na kubaki miili tu ikiishi.
Wanafikilia zaidi miili yao kuliko roho zao, kwao maisha ni kula na kuvaa! Basi. Ukichezea miili yao wanakasirika na kuumia, roho hawazijali sana kwa sababu walikwishazikatia tamaa.
Binadamu wa kawaida akiteswa kinyama kwa kukatwakatwa viungo vya mwili wake na kutobolewa macho, akatupwa chini akaachwa ayakabili maumivu ya kukienda kifo, hata akiokotwa, akagangwa kwa kuwekewa vilaka kwenye sehemu za mwili wake zilizochokonolewa kikatili, atapona makovu ya mwili lakini roho itabaki na vidondo vya ukatili ule na wakati mwingine roho inaweza kufa kabisa kwa kutokiogopa kifo.
Hivyo basi, wanapojitokeza wapumbavu wachache wasiojua maana na neno mpumbavu na kuanza kuzomoka kwa kuushambulia mwili usiokuwa na roho, wakiutuhumu kwa kulinda heshima ya miili inayoishi bila roho, hawa wanapaswa kujumuishwa kwenye genge la wahuni wanaojeruhi miili isiyokuwa na roho kwa vitu vyenye ncha kali.
Ni aina hii ya watu ambao kwa lugha nzuri ya kichokonozi wanaitwa wanafiki wanaoweza kumuona mfalme akitembea uchi, badala ya kumuambia bwana mkubwa unatembea ukiwa uchi ili abaini kuwa yu mtupu hivyo anapaswa kutafuta mavazi ya kusetiri utupu wake, wao wakiwa wameukodolea utupu huo hupiga makofi na kushangilia huku wakisema, mtukufu leo umependeza sana.
Ni aina hii hii ya watu walio jikoni mwa watawala wetu ambao wanaendelea kuwapotosha kwa kuwaaminisha kuwa vidonda walivyonavyo watanzania ndani ya mioyo yao dhidi ya ukatili wanaofanyiwa baadhi ya ndugu, rafiki na jamaa zao na watu wanaodaiwa kuwa maaskari kanzu ni vipele tu vinavyoweza kugangwa kienyeji kwa kutobolewa na kunyunyiziwa vumbi la mchanga.
Vidonda vya watu wa aina ya Dk. Stephen Ulimboka, ambaye licha ya kumtaja katili alimtenda ukatili uliopitiliza na kueleza mahali alipo wenye mamlaka ya kumkamata hawataki kumkamata.
Vidonda hivi huwa haviponi. Huuma sana nyakati zote na maumivu hayo ndiyo huwasukuma wanaoumizwa nayo kutafuta matabibu wa kuvitubu kwa kuwafukuza walioko madarakani; walioshindwa kuviponya na kuingiza utawala mpya kwa imani ya kuponywa.
Makuwadi wa wakubwa wanaofikisha ujumbe potofu kwao kuhusu mwenendo wa hao wanaowakuwadia, wanaliangamiza taifa letu kwa uongo wao. Kwa uongo wao wanawagombanisha wakubwa na wananchi wao.
Ndiyo hawa wanaojitokeza leo kushambulia miili yenye roho zilizokufa, inayohofia tamko la kutisha lililotolewa na Benard Membe, mtu mkubwa katika nchi yetu aliyeutangazia umma kuwa anao maadui 11 ambao siku akioteshwa na Mungu kuusaka ukubwa zaidi ya aliona sasa, watu hao atawashughulikia.
Membe anasuburi kuoteshwa na Mungu ili atekeleze ukatili na Mungu huyo atakayemuotesha lazima atakuwa Mungu wa manyani kwa sababu Mungu wa binadamu hawezi kumuotosha binadamu ndoto ambayo itamsukuma kwenda kuwaangamiza watu wanaoishi na roho zilizokufa kwa sababu hawatakubali, watajitetea katika unyonge wao.
Watajitetea ili walau kuponya miili yao isiangamizwe kama roho zao.
Sasa, matarishi wa kujitolea walionifikishia ujumbe wa kuogofya kwa sababu ya maandishi yangu ya kichokonozi wanapaswa kutambua kuwa wanahangaika na mwili wenye roho iliyokwishaangamizwa hivyo ujumbe wao nameusikia kwa  sababu mwili unayo masikio ya kusikia lakini siupokei kwa sababu roho inayopokea, haipo.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya