Thursday, December 26, 2024
spot_img

KUBENEA AANZA MAISHA MAPYA GEREZANI

 

Saed Kubenea

NA MWANDISHI WETU

Mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, Said Kubenea amekamatwa na kufikishwa mahakamani akituhumiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha.

Kubenea amekatwa na polisi Septemba 5, 2020 akiwa katika gari la abiria lenye namba ya usajili T 645 DKR  akitokea mpaka wa Namanga kuelekea Arusha.

Tayari Kubenea amekwishafikishwa mahakamani mjini Arusha na kusomewa mashtaka mawili, la kwanza kuingia nchini kinyume na sheria ya uhamiaji, sura ya 54 marejeo ya mwaka 2016 na shtaka la pili ni kuingiza nchini fedha za kigeni bila kutoa tamko kinyume na kanuni za utoaji tamko la fedha mpakani za mwaka 2016.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka, Biswalo Mganga, baada ya kukamatwa na kupekuliwa alikutwa na Dola za Marekani  USD (8000), Shilingi za Kenya 491,700. na shilingi za Tanzania 71,000.

Aidha, Kubenea alikutwa na tiketi ya basi ya la Super Coach, lenye namba za usajili KCP 4230 ya Septemba 5, 2020 ikionyesha kuwa siku hiyo alisafiri kutoka Nairobi Kenya hadi mpaka wa Namanga na pia alikutwa na hati ya makubaliano kati ya Hali Halisi ya Tanzania na Buni Media Limited  ya Kenya.

Vitu vingine alivyokutwa navyo ni  risiti ya malipo ya hoteli iitwayo After 40 Hotels Limited ya jijini Kenya ambayo ilikuwa imeandikwa jina lake kama mgeni aliyepanga kwenye hoteli hiyo kuanzia Septemba 3 hadi 5, 2020 pamoja na hati yake ya kusafiria.

“Mara baada ya kukamatwa, mtuhumiwa alieleza kuwa alifika mkoani Arusha tarehe 2/9/2020 akitokea Dar es Salaam na kufikia katika hoteli iliyopo Arusha mjini.

” Alieleza zaidi kuwa tarehe 3/9/2020 alikwenda kulala kwa kaka yake na tarehe 4/9/2020  alikwenda Namanga na kupokea fedha taslimu tajwa hapo juu kutoka kwa raia wa Kenya.

“Hata hivyo baada ya kupitia ushahidi uliokusanywa nimebaini kuwa mtuhumiwa Said Ahmed Kubenea hakufikia katika hoteli aliyoitaja Arusha mjini wala kulala kwa kaka yake kama alivyoeleza.

” Mtuhumiwa tajwa aliingiza nchini fedha za kigeni bila kutoa tamko rasmi la kisheria kinyume na masharti ya kanuni za The  Anti- Money Laundering ( Cross – Border Declaration of Currency and Bearer Negotiable Instrument) Regulations, 2016 zikisomwa pamoja na kifungu cha 28b (1) (a) cha sheria ya kuzuia utakatishaji wa fedha haramu Na. 12 ya mwaka 2006.” Inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Inasomeka zaidi kuwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Mganga kujiridhisha na uwepo wa ushahidi wa kutosha dhidi ya mtuhumiwa  pamoja na misingi ya kikatiba inayomuongoza mkurugenzi wa mashtaka kama ilivyoainishwa  katika ibara ya 59B (4) (a) hadi (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ameidhinisha Mashtaka dhidi ya Kubenea.

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya