TERESIA MHAGAMA
WAZIRI wa Nishati, Dk. Juma Homera, leo amezindua mifumo mipya ya kuhudumia wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mkataba wa Huduma kwa Wateja ulioboreshwa.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam na lengo lake ni kuwawezesha wateja wakubwa na wadogo wa kupata huduma kwa haraka na urahisi.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo, Dk. Homera amesema Tanesco imeonyesha kuwa imedhamira kuboresha huduma kwa wateja jambo lenye maslahi kwa taifa katika utekelezaji wa Dira na Maendeleo ya 2050.
Mifumo iliyozinduliwa na Dk. Homera ni ‘Twiga Assistant’ suluhisho la kisasa linalotumia akili mnemba (AI) na kumwezesha mteja kupata huduma saa 24 kwa siku bila kulazimika kupiga simu TANESCO na ‘Twiga Premium Portal’ jukwaa maalum la kidijitali litakalowawezesha wateja wakubwa kupata huduma mbalimbali kwa urahisi.
Aidha, Dk. Homera amezindua namba maalum 185 kwa ajili ya wateja wakubwa, itakayowawezesha kupata huduma za haraka, za moja kwa moja na zenye kipaumbele pamoja na uzinduzi wa kitengo cha huduma kwa wateja
wakubwa ili kuhakikisha kundi hilo linapata huduma zinazokidhi mahitaji yake.
Dk. Homera amelitaka shirika hilo kusimamia utekelezwaji wa mkataba wa huduma kwa wateja katika ngazi zote na ahadi zilizomo ambazo ni sehemu ya utamaduni wa kazi wa kila mtumishi. Amesisitiza kuwa mifumo yote iliyozinduliwa inapaswa kufanya kazi kwa ufanisi muda wote na itumike kwa vitendo ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.
