RIPOTA PANORAMA
NAIBU Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Namibia ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu na Petrus Tileinge Damaseb wa Namibia na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda Cheborion Barishaki wameteuliwa kuwa makamishna watakaochunguza wahusuka kutenda makosa ya jinai na kukiuka sheria Oktoba 29.
Majaji hao wawili wameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa miongoni mwa makamishna sita wa tume watakaochunguza waliohusika na makosa ya jinai kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Rais Samia alizindua rasmi tume hiyo jana, Ikulu ya Dar es Saalam na kuipa miezi mitano ya kufanya kazi ikiwa chini ya uenyekiti wa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shabani Ally Lila. Hata hivyo Rais Samia alisema muda huo unaweza kuongezwa endapo kutakuwa na sababu za msingi.
“Kama kutakuwa na ombi la kuongezewa muda, tutaliangalia baadaye,” alisema Rais Samia wakati wa uzinduzi uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Jaji Barishaki mbali ya Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda inayofanya kazi kama Mahakama ya Kikatiba ya Uganda pia ni Jaji wa Kitengo cha Rufani cha Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki
Makamishna wengine ni Jaji Mstaafu Gad John Mjemmas, Jaji Mstaafu Awadh Mohamed Bawazir na Jaji Mstaafu Aishieli Nelson Sumari.
Akizindua tume hiyo, Rais Samia aliwataka watanzania kushirikiana na makamishna ili waweze kutekeleza majukumu yao bila vikwazo.
“Niwasihi sana watanzania wote kutoa ushirikiano unaohitajika na tume katika kutekeleza majukumu yao. Tuisaidie tume hii iweze kufanya kazi yake na tusiisumbue,” alisema.

