RIPOTA MAALUMU
TANZANIA na Algeria zimekubaliana kuimarisha sekta ya kilimo nchini kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na kuendeleza wakulima wadogo kupitia uzalishaji na biashara endelevu katika soko la Algeria.
Makubaliano hayo yalifikiwa Agosti 4, 2026 kati ya Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde na Balozi wa Algeria nchini Tanzania, Ghalib Zermane, Julai 3, 2026, katika ofisi za Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo ya Silinde na Zermane yaliangazia fursa za biashara na uwekezaji, matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo na kuongeza thamani ya mazao, hususan katika tasnia za Kahawa na Ndizi.
Tanzania imekuwa ikiuza Kahawa katika masoko ya kimataifa kutokana na ubora wake na mfumo wa kisayansi wa upangaji wa madaraja, ambao hupunguza vihatarishi vya biashara na kuongeza ushindani wa kimataifa.
Kwa upande wake, Balozi Zermane alisema Algeria ni soko kubwa la bidhaa za kilimo, ikitumia takribani tani 130,000 za Kahawa kwa mwaka zenye thamani ya kati ya Dola za Marekani Milioni 600 hadi 700. Vilevile, matumizi ya Ndizi nchini humo hufikia tani 250,000 kwa mwaka zenye thamani ya takribani Dola za Marekani Milioni 250. Takwimu hizi zinaonesha kasi ya ukuaji wa soko la Algeria na kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa hizo katika miaka ya hivi karibuni.
Wengine walioshiriki katika mazungumzo hayo ni Mkurugenzi Mkuu Shirika la Mbole (TFC), Samuel Mshote, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Primus Kimaryo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao wa Wizara ya Kilimo, Dk. Yasinta Nzogela na Mwakilishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).

