Matokeo ya kufungwa 2-1 na England yanaweza kuumiza, lakini kwa namna DRC Congo walivyocheza, hakuna sababu ya kujiona wameshindwa vibaya.

Ukiangalia ubora wa kikosi cha England, tofauti ilikuwa wazi. England waliingia uwanjani wakiwa na wachezaji waliotoka kushinda mataji katika ligi kubwa za Ulaya.

Harry Kane ametwaa ubingwa wa Bundesliga akiwa Bayern Munich. Marcus Rashford ameshinda La Liga akiwa Barcelona. Declan Rice, Bukayo Saka, Eberechi Eze na Noni Madueke wametoka kwenye msimu wa ubingwa na Arsenal.

Hawa ni wachezaji waliozoea mechi za presha, hatua za mtoano na ushindani wa kiwango cha juu kabisa.

Lakini pamoja na tofauti hiyo ya uzoefu na ubora wa vikosi, DRC Congo hawakuwa wasindikizaji. Walipambana kwa ujasiri, waliwashtua England kwa bao la Wissa dakika ya 7 tu ya mchezo na kwa vipindi kirefu waliifanya England kutafuta ushindi kwa jasho kubwa.

Kufungwa kwa tofauti ya bao moja dhidi ya timu yenye nyota wa kiwango hicho si aibu.

Ni ishara kwamba soka la DRC Congo limepiga hatua na linaweza kushindana na mataifa makubwa duniani.

Ndiyo maana, DRC Congo hawapaswi kutoa hata tone la chozi. Wameondoka kwenye Kombe la Dunia, lakini wameondoka wakiwa wamejijengea heshima. Mara nyingine, matokeo hayaonyeshi ukubwa wa mapambano yaliyokuwa uwanjani.

Leo, DRC Congo wamepoteza mchezo, lakini wameonyesha kuwa Afrika inaweza kusimama kifua mbele dhidi ya yeyote

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here