.

Katika historia ya maendeleo ya sekta ya nishati Afrika Mashariki, kuna miradi michache yenye ukubwa na athari chanya zinazoweza kulinganishwa na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Mradi huu si tu unafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Uganda, bali pia unaibeba ndoto ya kuifanya Afrika kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani.

Kutoka kwenye visima vya mafuta vya Hoima nchini Uganda hadi mwambao wa Bahari ya Hindi katika eneo la Chongoleani,Mkoani Tanga, safari ya kutimiza ndoto ya kujenga bomba refu zaidi duniani la kusafirisha mafuta ghafi yanayohitaji kupashwa joto (heated crude oil pipeline) sasa imefikia hatua za mwisho za utekelezaji wa mradi huo.

Mradi wa East African Crude Oil Pipeline (EACOP) wenye urefu wa kilomita 1,443, ambapo kilomita 1,147 zipo Tanzania na kilomita 296 Uganda, ulianza kama wazo mwaka 2016 baada ya Tanzania kuchaguliwa kuwa njia ya kusafirisha mafuta ya Uganda kwenda soko la dunia kupitia Bandari ya Tanga.

Mwaka 2017, Tanzania na Uganda zilisaini Mkataba wa Serikali kwa Serikali (IGA), huku viongozi wa nchi hizo mbili wakiweka mawe ya msingi kuashiria mwanzo wa safari hiyo kubwa ya kihistoria. Mwaka 2022 ulifuatiwa na uamuzi rasmi wa uwekezaji (Final Investment Decision), hatua iliyofungua milango ya ujenzi kamili wa mradi huo.
Leo, miaka kadhaa baadaye, ndoto hiyo imekaribia kutimia.

Kupitia ziara ya Waziri wa Nishati nchini Mhe. Deogratius J. Ndejembi, amesema mradi wa EACOP umefikia asilimia 86 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2026 mwaka huu.

Akizungumza Juni 29, 2026 wakati wa ukaguzi wa mradi katika eneo la Chongoleani, Tanga, Waziri alisema maendeleo hayo yanaonyesha kasi nzuri ya utekelezaji, huku matarajio yakiwa ni kwamba meli ya kwanza ya kubeba mafuta ghafi itaondoka Bandari ya Chongoleani mwezi Januari 2027, hatua itakayofungua rasmi ukurasa mpya wa biashara ya mafuta Afrika Mashariki.

Mradi wa EACOP ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya miundombinu kuwahi kutekelezwa katika ukanda wa Afrika Mashariki ukiwa na thamani ya Dola za Marekani Bilioni 6.02.

Serikali ya Tanzania kupitia TPDC imechangia Dola za Marekani Milioni 374, sawa na asilimia 15 ya umiliki wa wanahisa, huku mradi ukihusisha pia wadau wengine wa kimataifa.

Mbali na lengo la kusafirisha mafuta kutoka Uganda kwenda soko la dunia, mradi huu umeendelea kuwa chanzo kikubwa cha ajira na uchumi kwa wananchi WA eneo hilo

Kwa mujibu wa Waziri Wa nishati Deogratius Ndejembi, zaidi ya ajira 10,000 zimezalishwa wakati wa ujenzi, ambapo Watanzania 7,500, sawa na asilimia 75, ndio walionufaika moja kwa moja WA Ajira hizo.

Pamoja na mafanikio hayo, Waziri Ndejembi amesema bado zipo changamoto chache zinazohitaji kukamilishwa, hususan ujenzi wa njia za umeme zitakazotumika kuendesha mitambo ya mradi.

Ameielekeza TANESCO kwa kushirikiana na mkandarasi kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kabla ya muda wa mkataba kuisha mwanzoni mwa Mwezi Agosti, ili kusiwepo na ucheleweshaji wa hatua za mwisho za mradi.

Kwa ukubwa wake, EACOP unatajwa kuwa bomba refu zaidi duniani la kusafirisha mafuta ghafi yanayopashwa joto, likiwa na uwezo wa kuunganisha uzalishaji wa mafuta wa Uganda na masoko ya kimataifa kupitia Bandari ya Tanga. Mradi huu umeifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara ya nishati katika Afrika Mashariki na umeongeza hadhi ya Bandari ya Tanga katika biashara ya kimataifa.

Kadiri Agosti 2026 inavyokaribia, macho ya Afrika Mashariki yanaendelea kuelekezwa Chongoleani. Kukamilika kwa EACOP hakutakuwa tu mafanikio ya ujenzi wa bomba la mafuta, bali pia alama ya ushirikiano wa kikanda, uwekezaji mkubwa na matarajio mapya ya ukuaji wa uchumi kwa Tanzania na Uganda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here