Aliyekuwa mke wa Rais wa zamani wa Korea Kusini, Kim Keon Hee, amehukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kupokea zawadi za thamani kwa njia isiyo halali, ikiwemo vito, mkoba wa kifahari wa Dior na saa ya gharama kubwa.
Mahakama ilisema Kim alitumia nafasi yake kama mke wa rais kuathiri baadhi ya maamuzi ya serikali, ikiwemo uteuzi wa watu katika nafasi mbalimbali na kutoa upendeleo kwa wafanyabiashara waliokuwa wakitafuta manufaa ya kisiasa.
Kesi hiyo imeongeza msukosuko mkubwa katika siasa za Korea Kusini, hasa baada ya mume wake, Rais wa zamani Yoon Suk Yeol, kuondolewa madarakani mwaka 2025 kufuatia jaribio lake la kutangaza sheria ya kijeshi lililozua mzozo mkubwa nchini humo.
Kwa wengi, hukumu hii imekuwa ishara nyingine ya namna viongozi na watu wenye ushawishi mkubwa wanavyoweza kuwajibishwa wanapokiuka sheria.






