.Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Serikali imepokea jumla ya mapendekezo 727 kutoka kwa wadau wa Serikali na Sekta Binafsi kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi, ada na tozo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza leo Juni 5, 2026, jijini Dodoma wakati wa vikao vya Kamati za Ushauri (Think Tank Committees) kuhusu Sera za Kodi vilivyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage, Treasury Square, Balozi Omar alisema mapendekezo hayo yamechakatwa kwa lengo la kufanya maboresho katika sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu kodi, ada na tozo.
Alieleza kuwa ushirikishwaji wa wadau katika mchakato wa maandalizi ya bajeti ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya uwazi na uwajibikaji wa Serikali, pamoja na kuimarisha ushiriki wa wananchi na sekta binafsi katika kupanga na kuendesha uchumi wa nchi.
Balozi Omar alisema hatua hiyo pia inalenga kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini, kuongeza ushindani wa kiuchumi na kuchochea ukuaji wa uchumi unaowanufaisha wananchi.
Aidha, alibainisha kuwa mkakati wa Serikali ni kukuza uchumi, kuhamasisha uwekezaji, kuendeleza sekta ya viwanda vya ndani na kupunguza utegemezi wa misaada pamoja na mikopo katika utekelezaji wa bajeti za maendeleo.
“Katika mwaka ujao wa fedha, Serikali imekusudia kutekeleza zaidi ya asilimia 75 ya bajeti yake kwa kutumia mapato ya ndani,” alisema Balozi Omar.
Vikao hivyo viliwashirikisha viongozi na wadau mbalimbali kutoka Serikali na Sekta Binafsi, huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo ikiwakilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil.
