Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imesema zaidi ya miti 94,000 imepandwa katika Mradi wa Barabara ya Mzunguko wa Nje wa Jiji la Dodoma (Ring Road) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Taarifa hiyo imetolewa na Meneja wa Mazingira na Jamii wa TANROADS, Bi. Zafarani Madayi, mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, alipotembelea banda la Wizara ya Ujenzi na TANROADS katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.
Bi. Madayi alisema kuwa Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na TANROADS inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira, ikiwemo Mradi wa Kukijanisha Jiji la Dodoma (Green Spine Project – GSP), unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia African Development Bank.
Alifafanua kuwa kupitia mradi huo, ukanda wa kijani umeanzishwa kuzunguka Barabara ya Mzunguko wa Nje wa Jiji la Dodoma, ambapo hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu miti zaidi ya 94,000 imepandwa kwa lengo la kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji unaendelea sambamba na zoezi la upandaji miti, huku ukihusisha usimikaji wa matanki ya maji pamoja na uchimbaji wa visima 11 vitakavyowezesha matumizi ya mfumo wa umwagiliaji wa matone ili kuhakikisha miti iliyopandwa inastawi na kudumu.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 kimewakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira kutoka taasisi, mashirika, wizara na wananchi kwa ujumla chini ya kaulimbiu isemayo, “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”
