Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imeingia katika hatua mpya ya mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kuimarisha ushindani katika soko la kimataifa kupitia upanuzi wa fursa za uwekezaji, uimarishaji wa msingi mpana wa uchumi na ujenzi wa mazingira rafiki kwa maendeleo endelevu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 04 Juni 2026, alipofungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji Zanzibar 2026, lililofanyika katika Golden Tulip Airport, likiwakutanisha wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu, mageuzi ya taasisi na matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuongeza ushindani wa Zanzibar katika soko la kimataifa na kuvutia mitaji zaidi.
Aidha, amebainisha kuwa zaidi ya miradi 800 ya uwekezaji yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 9 inaendelea kutekelezwa visiwani humo, huku uchumi ukikua kwa asilimia 7.3 na mfumuko wa bei ukidhibitiwa katika kiwango cha asilimia 4.1.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi alishuhudia utiaji saini wa mikataba ya ushirikiano kati ya Zanzibar Investment Promotion Authority (ZIPA), taasisi ya wawekezaji ya Marekani pamoja na Benki ya Afreximbank, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuongeza kasi ya uwekezaji Zanzibar.
Jukwaa hilo limewakutanisha takribani washiriki 600 kutoka mataifa mbalimbali duniani wakiwemo wawekezaji, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo, wafanyabiashara pamoja na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora), likiwa ni sehemu ya mikakati ya kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha uwekezaji katika Afrika Mashariki.
